Lema ajitosa DP World

Mwenyekiti wa chadema kanda ya kaskazini Godbles Lema akizungumza kwenye mkutano wa hadhara



Arusha. Mwenyekiti wa chadema kanda ya kaskazini God bless Lema ameitaka serikali kujitokeza hadharani kujibu hoja za wananchi juu ya uwazi wa sakata la bandari badala ya kujificha kwenye kichaka cha dini.

Alisema kuwa usiri kwenye mkataba wa ushirikiano wa uendeshaji bandari kati ya kampuni ya DP World na Tanzania unazidi kutoa mashaka wananchi hivyo serikali kukaa kimya au kutoa majibu mepesi yanayoegemea dini yanaweza kuzua mgogoro mkubwa baadae katika utekelezaji wake na kuigharimu serikali zaidi mbele ya vyombo ya kisheria au fidia.

Lema aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara wa kuzindua operesheni ya "tutambuane kidijitali" unaohamasisha wakazi wa kanda ya kaskazini kujisajili kupitia app maalum waliyoitengeneza.

"Kwenye mkataba huu sioni tatizo la mwarabu kuja kuwekeza hapa Tanzania, tatizo ni uwezo ndogo wa viongozi wa chama cha mapinduzi kujadili maswala ya biashara"

Lema alisema kuwa kasoro ya kwanza wanayoiona ni kuitegemea kamati ya bunge pekee kwenda kufanya tathimini badala ya serikali kutafuta washauri wakubwa wa maswala ya kibiashara na uchumi  duniani na kuwagharamia Ili kuja kutengeneza muhtasari mzuri wa mkataba.

"Nchi imepigwa kwa sababu ya kujua Kila kitu, hatutaki kujifunza, kwenye swala hili tungetafuta washauri wa maswala ya biashara na uchumi duniani watusaidie kujua kasoro hizi kabla ya kusaini mkataba...halafu wananchi tukiuliza watawala wanageuza kuwa maswala ya kidini" alisema Lema na kuongeza...

"Naomba wananchi wenzangu msijadili Wala kuingia mkenge wa kujadili siasa za nchi hii kwa kutumia dini,  hakika mtaikatakata hii nchi maana hakuna kitu kina nguvu kama dini duniani" 

Lema aliwataka wakazi wa kanda ya kaskazini kuacha kumchukia Rais Samia kwa kigezo cha kutoka Zanzibar bali waichukie chama chake kwa matendo wanayoyafanya.

"Niwaombe msimchukie Rais Samia kwa sababu anatoka Zanzibar, naye ni kama watu wengine bali chukieni kwa matendo yao hasa ya wizi waliyoiba serikali za mitaa na majimbo hadi urais na njia ni moja tu ya kuwafuta katika uchaguzi ujao na tumekuja kuwahamasisha mjisajili na app maalum yetu tutambuane na kufanya harakati zetu"

Kwa upande wake katibu wa Chadema kanda ya kaskazini, Amani Golugwa alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kuzindua operesheni ya kutambuana kidijitali kwa lengo la kuwafikia watanzania wengi zaidi watakaokuwa wanachama wa chama hicho.

"Upo utaratibu ambao tumeutengeneza wa chama chetu ambao watajisajili kidijitali kupitia app maalum ya 'chadema ambayo wananchi wataingiza taarifa zao muhimu na atalipa ada na kujiunga uanachama na kupata kadi maalum"

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwafikia watu wengi ambao watafanya harakati za kukirudishia chama hicho heshima yake ya kurudisha majimbo yao waliyopotea lakini pia watakaokuwa mstari wa mbele kupigania haki na maslahi ya Taifa.

 
Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!