Na Bertha Mollel
Arusha. Katibu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati jijini Arusha, John Tanaki amejitosa kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya wajumbe kumkubali kuipeperusha bendera ya CCM katika Jimbo la Arumeru Magharibi.
Akichukua fomu hiyo, Tanaki amesema azma yake kubwa ni kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo iwapo atapata uteuzi ndani ya Chama Chake.
Tanaki ambaye ni Msomi wa Chuo Kikuu amesema lengo la kujitosa kwenye nafasi hiyo ni kutumia haki yake ya msingi, na kikatiba kuwatumikia wananchi wa Arumeru Magharibi huku akiomba ridhaa ya uteuzi kupitia chama chake cha Mapinduzi CCM.
"Nimefika ofisi za chama chetu kuchukua fomu kutia nia nafasi ya ubunge, na kinachonisukuma ni kuwatumikia wananchi wa jimbo la Arumeru Magharibi na ninandoto ya kuifanya dunia kuwa sehemu salama" amesema muumini huyo mzuri katika dini ya kikristo.
Alisema iwapo atateuliwa kugombea jimbo la Arumeru Magharibi atatumikia vema wananchi katika jimbo hilo na kuwahakikishia kutojutia uamuzi wao.