Na mwandishi wetu
Arusha. Kampuni ya Petro Africa (T) Ltd imefanikiwa kufanya uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa kituo cha mafuta wilayani Longido kilichogharimu zaidi ya shilingi milioni 800.
Uwekezaji huo uliofanyika katika kata ya kimokouwa, umehusisha visima vya kuhifadhia mafuta, pampu za kisasa, maeneo ya maegesho, ofisi za kisasa, pamoja na miundombinu ya usalama.
![]() |
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Ismail Ussi akikagua visima vya kituo cha mafuta cha Petro Africa (T)Ltd |
Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa PetroAfrica (T) Ltd, Abdi Hassan Ibrahim amesema kuwa mradi huo uliotekelezwa kwa miezi 14 pekee (March 2024 hadi june 2025) una lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa mafuta kwa wananchi na sekta ya usafirishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo la mpaka wa Namanga.
Ibrahim ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa kituo cha mafuta baada ya kutembelewa na msafara mzima wa mbio za mwenge wa uhuru uonaoongozwa na Mkimbiza mwenge kitaifa Ndugu Ismail Ally Ussi.
Ametumia nafasi hiyo kuishukuru serikali kwa kuweka mazingira mazingira mazuri hadi kufanikisha mradi huo.
Amesema mradi huo mbali na kuongeza huduma ya nishati, pia wamesaidia taasisi za umma na binafsi kupunguza changamoto za upatikanaji wa mafuta na zaidi wametoa ajira kwa wananchi wa Longido .
amesema kuwa kituo hicho ni cha kipekee katika mkoa wa Arusha na kimejengwa kwa kuzingatia usalama, ufanisi na urafiki kwa mazingira.
Baada ya kukagua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndugu Ussi, amesifu mradi huo na kuzitaka sekta zingine za binafsi nchini kuchangamkia maboresho makubwa ya sera ya uwekezaji kuwekeza miradi mingi nchini.
Amesema kuwa serikali ya awamu hii imefanya kazi kubwa ya kuondoa vikwazo vingi vya uwekezaji ili kuvutia wadau wengi kufanya kazi na biashara hivyo ni vema wote kunufaika nao
Ussi amesema kuwa kuwa mradi huo ni ushahidi wa namna sekta binafsi inavyoweza kushiriki kikamilifu katika jitihada za kitaifa za maendeleo.
“Nawapongeza kwa uwekezaji huu wa mfano kwani mmeonesha uzalendo wa hali ya juu na mmejitokeza kuwa sehemu ya historia ya Mwenge wa Uhuru kwa vitendo”amesema na kuongeza;
“Hii ni njia mojawapo ya kumuunga mkono Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, hivyo niwaombe na wengine wahakikishe wanatumia fursa hii vuzuri” amesema Ussi.
Mbali na hilo, Ussi amewataka wananchi wa wilaya ya Longido kuwaunga mkono wawekezaji wanaojitokeza kutatua kero mbalimbali katika jamii zao ikiwemo kununua bidhaa wanazoleta ili kuwatia moyo kufanya mambo mengine makubwa zaidi.
“Hapa amejitokeza muwekezaji huyu kajenga kituo hiki ambacho kitaondoa kero ya upatikanaji wa mafuta, niwaombe mje kununua mafuta hapa, maana hadi kuita mwenge wa uhuru kuzindua maana yake mafuta yake yako safi na yana viwango vya hali ya juu” amesema.
Pia ametoa wito kwa viongozi wa wilaya pamoja na wananchi kuunga mkono juhudi za wawekezaji kama PetroAfrica, kwa kuwapa ushirikiano, kuwaheshimu na kuwatangaza kama mabalozi wa maendeleo katika jamii
“Tukiwaunga mkono wawekezaji wetu wa ndani, tunamuunga mkono pia Rais katika kutekeleza dira ya taifa ya uchumi wa viwanda. Huduma zinazotolewa ni lazima zizingatie viwango, vigezo, na weledi ili ziwanufaishe wananchi kwa ubora unaotakiwa,” alisisitiza.
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Meijo Noah amesema kuwa kituo hicho kitasaidia wananchi wengi wenye vyombo vya moto ambao wamekuwa wakiteseka kutafuta huduma ya mafuta hasa wenye magari binafsi na bodaboda za biashara