Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi amewabebesha majukumu mazito viongozi wa dini na viongozi wa mila katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha, kuhakikisha wanalinda na kuombea amani na utulivu nchini.
Kihongosi ametoa jukumu hilo katika ziara yake ya kujitambulisha katika wilaya ya Longido ikiwa ni siku nne pekee tangu kukabidhiwa ofisi hiyo rasmi baada ya uteuzi.
Kihongozi amesema kuwa amani na utulivu ulioko nchini ndio unaozalisha fursa za kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji na biashara hivyo kuwataka viongozi hao kuendelea kuiombe nchi ibaki na tunu hiyo kwa maendeleo ya sasa na vizazi vijavyo.
“Niwaombe kila mmoja aone ana wajibu wa kulinda amani na usalama wetu, tena tusiruhusu kwa namna yoyote mtu akajaribu kuvuruga kwani bila amani hakuna utulivu wa kufanya maendeleo yoyote” amesema.
“Tukivuruga amani yetu tutakuwa wakimbizi katika nchi za watu wengine, na tusijaribu kufanya hivyo tena tujifunze yanayoendelea katika nchi jirani, kila mmoja ana macho, anaona na anatambua kwamba kuna nchi hazijatulia na wanatamani na nchi yetu iharibikiwe basi tusifanye hivyo ndugu zangu” amesema.
Mbali na hilo, Kihongosi amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kupuuza baadhi ya vyama vya siasa vinavyodai hakuna uchaguzi kwa kutumia kauli ya 'No Reform No Election' wakimaanisha 'bila mabadiliko hakuna uchaguzi'.
“Katiba ya nchi yetu inasema kila baada ya miaka mitano kuna uchaguzi, sasa kuna watu wanasema No Reform NO election, wapuuzeni ndugu zangu, hiyo haipo maana kuhairisha uchaguzi ni kukiuka katiba yetu Tanzania, na tukikiuka katiba madhara yake ni makubwa sana” amesema.
“Hivyo niwaambie uchaguzi upo na serikali imejiandaa, Wananchi wamejiandaa na vyama vimejiandaa, hivyo chama kimoja kama kimeamua hakishiriki hakiwezi kukiambia vyama vingine visishiriki au wananchi wasishiriki” amesema.
Amewataka viongozi mbalimbali wa mkoa wa Arusha kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupigia kura wagombea waliojitokeza kwa amani na utulivu bila vurugu.
“Mama yako amekuzaa akutegemee umuhudumie, usijaribu kuandamana kwa sababu ya watu wachache wenye tama ya madaraka kwani hayo madaraka yapo tu na yanaweza kupatikana kwa amani na utulivu sio kwa fujo wala vurugu bali diplomasia” amesema.
Mwisho…