Rc Kihongosi atupa jiwe gizani, awapiga ‘STOP’ wambea ofisini kwake, akataa fitina, unafki na maneno ya uchonganishi



Ataka aachwe afanye kazi yake 

 

Arusha.  

Arusha. Mkuu mpya katika Mkoa wa Arusha Kenani Kihongosi amewapiga marufuku watendaji na watumishi kwenda ofisini kwake kupeleka maneno ya uongo na uchonganishi dhidi ya watumishi wenzao wa umma.

Kenani amesema kuwa yeye si muumini wa maneno ya chuki na unafki yenye mlengo wa kutengenezeana ajali kazini bali anatamani watumishi hao waishi kwa kupendana na kuoneana huruma na kusaidiana.

“Sipendi kuletewa maneno ya umbeya, usije kwangu unaniambia yule kiongozi ni m’baya sana au Mkurugenzi au Mkuu wa wilaya fulani ni mbaya sana, tafadhali niacheni, mimi ni kijana nina uwezo wa kuwajua watu kwa kufanya nao kazi kuwa nani mzuri na nani sio mzuri usinifundishe” amesema na kuongeza;

“Arusha mimi sio mgeni, najua mtakuja kuniaminisha kiongozi fulani hafai kumbe wewe ndio shida, sasa niwaambie wazi kuwa friji langu haligandishi, Ukileta maneno nitamuita huyo mwenzio nitakuamuru useme upya tukiwa pamoja ili tumalize fitina” amesema Kihongosi.

Kihongozi ameyasema hayo wakati wa kujitambulisha kwa watumishi mbalimbali wa Mkoa wa Arusha ikiwa ni siku chache tangu kuteuliwa kuja kuhudumu Mkoani hapa akitokea Mkoa wa Simiyu.

Amewataka watumishi hao kuishi kwa amani na upendo tena kwa kuoneana huruma na kusaidiana bila kutengenezeana ajali katika maeneo ya kazi zao.

 “Katika uongozi wangu asiwepo mtu akajiona yeye ni bora kuliko mtu mwingine, kila mmoja amepewa fursa na dhamana ya kufanya kazi kwa kipindi fulani , na baadae utaondoka na mwingine atakuja hivyo hatuna sababu ya kusemeana vibaya, kumchafua mwingine uonekane wewe ni bora,  hakuna sababu ya kutengenezeana ajali au kunyoosheana vidole bali kazi yako itakutambulisha uzuri wako”.

“Nasema hivyo kwa sababu, huna sababu ya kupeleka majungu, unafki chuki ili mwingine aonekane mbaya, Kikubwa tusimamie kanuni, mingozo, taratibu na  sheria ambazo zipo kutuongoza katika kufanya kazi zetu lakini tusisahau kuipa nafasi busara”.

Amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote kusimamia haki za watumishi wao na kuhakikisha zinapatikana kwa wakati ili kusaidia utekelezaji wa majukumu ya kuleta maendeleo kwa wananchi kuwa mepesi.

“Viongozi wenzangu wakiwemo Wakuu wa wilaya tujifunze kutendea haki wengine, asiwepo wa kuonewa wala kupendelewa bali mwenye haki apewe na siye na haki asipewe haki kwani Misingi ya haki  itatusaidia kutawala vizuri”

“Asikuambie mtu pengo lako halitazibika, hakuna pengo lisilozibika duniani,akifa mwingine mkeka jioni umetoka anakuja mwingine hivyo tusijipe umuhimu na kuwa bora kuliko mwingine yoyote, binadamu wote ni sawa hivyo watumishi wa umma heshimuni watu kwani haipunguzi cheo” amesema.

 


Mwisho….


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!