Arusha. Wafugaji Wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha wameiomba serikali kufanya utafiti wa dawa ya ugonjwa wa kizunguzungu unaosababisha idadi kubwa kubwa ya vifo vya mifugo yao.
Ugonjwa huo kitaalamu unajulikana kama ‘Coenurosis' unaosababishwa na minyoo aina ya Taenia multiceps, imekuwa ikisababisha kila mfugaji wilayani Ngorongoro kupoteza mbuzi na kondoo zaidi ya 40 kwa mwaka.
Kutokana na hilo, wafugaji hao wameiomba serikali kupitia taasisi zake kufanya utafiti wa tiba wa ugonjwa huo ambao bado hauna tiba.
Wafugaji hao wametoa kilio hicho mbele ya waziri wa mifugo na uvuvi Dr Ashantu Kijaji wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo katika wilaya ya ngorongoro Mkoani Arusha.
Akizungumza katika mkutano huo, m'bunge wa Ngorongoro, Emmanuel Shanghai amesema kuwa kila mfugaji amekuwa wakipoteza mbuzi na kondoo zaidi ya 40 kwa mwaka kutokana na ugonjwa huo ambao kwa kimasai wanauita 'Ormilo' wakimaanisha ugonjwa wa kizunguzungu.
"Ugonjwa huu ambao huonekana zaidi mwezi February hadi machi kuelekea kipindi cha mvua za masika, hudhoofisha mifugo yetu kwa kukosa hamu ya kula na kupata kizunguzungu kizungu cha mara kwa mara na ndani ya siku tatu hadi nne hufa"
"Tunaomba serikali ifanye mpango wa kututafutia dawa kwani kipindi cha kuelekea masika ambacho kuna malisho ya uhakika ndio tunapoteza mifugo yetu mingi badala ya kufaidi matunda ya kazi zetu" amesema M'bunge huyo.
Nae mfugaji Altapwai Mayanga amesema kuwa hofu yao kubwa ni ugonjwa huo kuwapata binadamu endapo hautazibitiwa kutokana na wafugaji wengi wakiona dalili za mfugo kupata ugonjwa huo huuza katika mabucha ya nyama.
Mkurugenzi wa huduma za mifugo Tanzania, Dr Benezeth Lutege amesema kuwa ugonjwa huo bado hauna tiba na unaweza kuua mbuzi na ng'ombe ndani ya siku saba hadi 14 atakapoanza kuonyesha dalili za kizunguzungu.
"Ugonjwa huu wa 'Coenurosis' hutokana na minyoo ambao huleta madhara kwenye utumbo wa mbuzi na kondoo watakapokomaa na kutaga mayai ambayo hukimbilia kwenye ubongo na kusababisha uvimbe wenye kuleta kizunguzungu kisha kufa.
"Hadi sasa ugonjwa huu hauna dawa wala tiba, zaidi tunawahamasisha wafugaji kuwapa dawa ya minyoo mara kwa mara mifugo yao ili kuepuka minyoo hao kukomaa tumboni mwa mifugo yao na kuleta madhara"amesema.
Amesema hadi sasa ugonjwa huo umesambaa katika Mkoa wa Arusha katika Wilaya za Ngorongoro, Monduli na Longido huku Mkoa wa manyara ukiwa katika Wilaya za Simanjiro Kiteto na Babati vijijini.