Arusha.
Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa maegesho ya magari katika mpaka wa Namanga ulioko Longido Mkoani Arusha.
Ujenzi huo unaotarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu, unatarajia kupunguza kero ya foleni na msongamano wa magari katika eneo la mpaka, kuboresha huduma za usafiri na biashara kati ya Tanzania na Kenya.
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kali amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuboresha miundombinu ya mipakani ili kurahisisha shughuli za forodha, kuongeza mapato, na kuvutia wawekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Maegesho hayo mapya yatakayokuwa na miundombinu ya kisasa pia yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi magari mengi kwa wakati mmoja ikiwa ni pamoja na malori ya mizigo yanayopeleka mizigo Uganda, Kenya, Somalia na kwingineko”amesema Kali.
“Tunafanya hivi kwa sababu Namanga imekuwa chachu kubwa ya mapato ya Wilaya yetu, ndio maana hata Rais Samia ameamua kutuletea shilingi Bilioni moja kujenga maegesho hayo kama sehemu ya kuboresha huduma na sisi tumejipanga kuwahudumia wafanya biashara wetu vizuri kwani wamekuwa neema kubwa kwetu” amesema.
Amesema kuwa wilaya ya Longido pekee imekuwa na makusanyo ya zaidi ya Sh11 hadi Sh14 bilioni mwa mwezi yakichagizwa kwa kiasi kikubwa na biashara zinazofanyika katika Mpaka huo.
Deo Gidio mfanyabiashara wa mazao katika mpaka wa Namanga ameipongeza serikali kwa hatua hiyo, akisema kuwa itasaidia si tu katika kupunguza msongamano bali pia kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo la mpaka.
Mwisho…