Arusha
Mwenge wa uhuru umetia kiti rasmi ndani ya Mkoa wa Arusha kupitia lango la Malula eneo la King'ori Kibaoni, Wilaya ya Arumeru, asubuhi ya leo Julai 05, 2025.
Ukiwa Mkoani Arusha, mwenge huo utakimbizwa umbali wa Kilomita 1,203.17 ndani ya Wilaya 6 na Halmashauri 7 za Mkoa wa Arusha ukianzia Meru, Arusha DC, Longido, Ngorongoro, Monduli na Arusha jiji.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi amesema jumla ya miradi 54 itapitiwa na mwenge huo zenye thamani ya Shilingi Bilioni 30.3.
Kenani amesema hayo, wakati akipokea rasmi mwenge wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu.
"Katika miradi hiyo 54, miradi 18 yenye thamani ya Sh12 bilioni itawekewa mawe ya msingi, miradi 4 yenye thamani ya Sh378.2 milioni itafunguliwa, miradi 19 yenye thamani ya sh 15.2 bilioni itazinduliwa na miradi 13 yenye thamani ya Sh 2.6 bilioni itatembelewa" amesema.
Hapo hapo Kihongosi alimkabidhi Mwenge huo wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mwinyi Ahmed Mwinyi kianzisha safari katika wilaya ya Meru chini ya kauli mbiu "Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa Amani na Utulivu".