Maagizo mapya ya serikali kwa Wakuu wa wilaya na wakurugenzi nchini

 


Arusha. Serikali imewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri kote nchini kuyapima maeneo yote yaliyoainishwa ni ya wafugaji ili yakatiwe hati.

Lengo ni kuyaweka katika ramani ya mpango wa matumizi bora ya ardhi, kuyawekea miundombinu ya kifugaji lakini pia kuyalinda maeneo hayo na matumizi mengine.

Hayo yamesemwa na Waziri wa mifugo na Uvuvi Dk Ashantu Kijaji wakati akizindua kampeni ya Chanjo na utambuzi wa mifugo Mkoani Arusha katika wilaya ya Longido.



“Wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kote nchini, hakikisheni maeneo yote ya serikali yaliyotengwa au kuainishwa ni ya wafugaji yapimwe na sisi wizara tumejitolea kuyakatia hati na yataandikwa maeneo ya wafugaji”

“lengo ni kuyatengenezea mpango mzuri wa matumizi kwenye maeneo hayo na kuyawekea miundo mbinu yote ya kifugaji ili wafugaji sasa wafuge vema na tunufaike na rasilimali bora kabisa tulizonazo nchini” amesema Kijaji.

Amesema hatua hiyo itapunguza migogoro ya ardhi hasa ya wakulima na wafugaji ambao wamekuwa wakiingiliana maeneo kwa ajili ya shughuli zao.

“Hapa nchini maeneo ya wakulima yapo lakini tukijiuliza maeneo ya wafugaji yako wapi, unakosa jibu, sasa Rais Samia amesema imetosha, kuanzia sasa wafugaji watakuwa na maeneo yao maalum na watapewa ruzuku za mbegu za mifugo na malisho na zaidi watapewa mbegu za madume”

“Lengo ni kupandisha thamani ya mifugo yetu na kuwa na sifa katika masoko ya kimataifa kwa ajili ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla”



Ametumia nafasi hiyo kuwataka wafugaji wote mkoani Arusha kuhakikisha wanakwenda kuchanja mifugo yao kwa ajili ya kujihakikishia usalama wao na kusaidia serikali kutambua idadi na taarifa za mifugo iliyoko nchini.

Awali m’bunge wa Longido Steven Kiruswa ameishukuru serikali kwa chanjo hiyo ambayo itasaidia kuwanusuru mifugo yao na magonjwa mbalimbali.

Pia ameiomba serikali kurudisha eneo zaidi ya eka 1000 analomiliki mmoja wa wawekezaji katika kata ya tingatinga  kwa ajili ya utalii wa picha  ili iwasaidie wafugaji kupata eneo la malisho.


Mkuu wa mkoa wa Arusha Kenani Kihongosi amewataka wafugaji hao kubadili mfumo wa shughuli hiyo kimazoea na kuja kibiashara ili kuweza kunuafaika na rasilimali hiyo muhimu.

Aidha kampeni hiyo ya chanjo ya mifugo kitaifa, inaenda sambamba na utambuzi wa mifugo kielekroniki kwa miaka mitano (2025-2029) kwa gharama ya Sh216 bilioni kwa lengo la kuboresha mazingira ya kifugaji na uchumi wa wafugaji kupitia masoko ya kimataifa yanayonunua mifugo na bidhaa zake.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!