Mnada wa bajaji waja Arusha




Arusha. Mamlaka ya udhibiti wa usafiri Ardhini (Latra), imesema kuwa wameanza mchakato wa kuomba ruhusa ya mahakama ya kuzipiga mnada bajaji zote zitakazomatwa zaidi ya mara moja zikiendesha shughuli zake bila leseni ya usafirishaji.


Hayo yamesemwa na ofisa mfawidhi wa Latra, mkoa wa Arusha, Amani Mwakalebela alipokuwa azingumzia juu ya suluhu ya mgomo wa daladala ulianza alfajiri ya julai 3, 2023  unaoshinikiza kuziondoa bajaji kwenye barabara wanazohudumu.

Alisema kuwa ndani ya Arusha kuna zaidi ya Bajaji 2000 zinazofanya kazi, wakati zilizosajiliwa hazizidi 350.

"Kama mnavyojua awali waliokuwa wanatoa lesseni za usafirishaji ni halmashauri ya Jiji la Arusha, lakini tangu mwaka jana tulikaa na tukaamua tufunge Usajili mpya baada ya kuonekana zimekuwa nyingi lakini nashagaa pamoja na kufunga bado kuna baadhi ya wafanya biashara wameendelea kuzinunua na kuziingiza katika mzunguko" alisema

Alisema baada ya kuona hivyo waliamua kufanya operesheni maalum ya kuzikamata na kuzipiga faini huku wakiwataka wahamie maeneo mengine ikiwemo miji isiyo na bajaji kabisa lakini wamekaidi.

"Sio kwamba hatukamati au kuwapa adhabu tunafanya hivyo lakini hawasikii, mtu Leo analipa faini kesho yuko barabarani hivyo tumeanza mchakato wa mahakama kuomba oda ya kuzichukua kabisa zisiwepo kwenye mzunguko na kuzipiga mnada mbali kabisa" alisema


 ofisa mfawidhi wa Latra, mkoa wa Arusha, Amani Mwakalebela


Mwakalebela alitumia nafasi hiyo kuwaomba madereva wa daladala kupitia uongozi wao kurudi barabarani na kuendelea kutoa huduma wakati swala hilo linaendelea kufanyiwa kazi huku akiwataka wafanya biashara wa bajaji wasio na leseni kuziondoa katika mzunguko wa usafirishaji ndani ya Jiji la Arusha.

Akizungumzia mgomo wao, mmoja wa madereva Emmanuel Swai alisema kuwa wameamua kugoma kutokana na uonevu mkubwa unaofanywa na mamlaka za usafirishaji ikiwemo kuziruhusu bajaji kufanya kazi yao tena kwenye ruti wanazotoa huduma hasa barabara za uswahilini-Dampo, Sombetini-ngusero, Majengo pamoja na na Patel-kwa mrombo.

usafiri m'badala


"Awali makubaliano ilikuwa ni bajaji wanakaa eneo moja kama taksi wakodishwe wapeleke watu mahali lakini sasa hivi wanafanya kazi ya kuokota abiria kama sisi wa daladala, tena wanakaa kwenye maegesho zetu na zaidi wanapita zile zile ruti tunazopita kitendo ambacho wanatuharibia biashara"

Akizungumzia mgomo huo, mwenyekiti wa chama cha wasafirishaji mkoa wa Arusha na Kilimanjaro(AKIBOA), Locken Adolf alisema kuwa utitiri wa bajaji umeathiri biashara ya daladala hivyo wanaiomba serikali kuzipunguza

"kwa ukubwa wa eneo la Arusha,  hazitakiwi kuzidi zaidi ya 100 lakini sasa zimekuwa nyingi na zimekuwa kero sana kutokana na zimeteka ruti zote za daladala na zinafanya biashara ya kuokota abiria kama wanavyofanya wenzao jambo ambalo sio makubaliano wakati zinaingia mjini"

Alisema kuwa katika ufuatiliaji wamebaini bajaji nyingi ndani ya Jiji la Arusha hazina leseni lakini zinaruhusiwa kufanya kazi tofauti na daladala ambazo zimekuwa zikipigwa faini kila hatua.

"Tunataka kujua anaeendesha usimamizi wa hizi bajaji ni nani na ana sauti gani kwenye mamlaka za serikali zinazosimamia usafirishaji maana wao wanafanya kazi kinyume na Sheria, taratibu na  makubaliano lakini hawafanywi chochote wanazidi kupeta tu"


Akizungumzia hali hiyo, Amina Hassan alisema kuwa mgomo huo ulianza leo alfajiri umesababisha mateso makubwa kwa wakazi wa Jiji la Arusha pamoja na wanafunzi wanaotumia usafiri huo kuwahi makazini na shuleni.


"Tunaomba serikali itafute suluhu la jambo hili kwani tunaoteseka ni wananchi na hili jambo la daladala kugoma imekuwa sio mara moja"

Ramadhani Ally aliiomba serikali kusikilizwa madai ya daladala endapo yana mantiki wapewe suluhu na kama hayana basi waondolewe  na usafiri wa magari makubwa aina ya Costa ziletwe zichukue nafasi yao.


"Shida hawa daladala wanataka wao wenyewe ndio wafanye kazi ya usafirishaji wakati hii ni biashara huria, inafaa Kila mtu acheze kwenye nafasi yake kupata kipato hivyo tunaomba serikali isikize madai yao kama yana maana watatuliwe lakini kama ni haya ya ubinafsi wenzao wasifanye kazi basi  wanaohamasisha mgomo wafutiwe leseni"

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!