Bethy Mollel -Arusha
Kikao cha Kamati ya ushauri ya Maendeleo katika halmashauri ya wilaya ya Arusha vijijini (Arusha DC) kimepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya mapato na matumizi ya Sh 68 Bilioni kwa mwaka 2025/2026.
Kikao hicho kimepitisha rasimu hiyo jana January 30,2025 baada ya mapitio ya mpango na bajeti kwa Mwaka 2023/2024 na ile ya 2024/2025 na kuamua kwa kauli moja Sh 68 Bilioni iwe ndio Makisio ya bajeti yao kwa mwaka 2025/2026.
Awali akizungumza katika kikao hicho mwenyekiti ambae pia ndio Mkuu wa Wilaya ya Arumeru DC Amiri Mkalipa amewataka wajumbe hao kutoa ushauri na mawazo yenye tija kuhusu Mpango na Bajeti hiyo kwa lengo la kuboresha huduma kwa jamii wanaowahudumia.
"Pamoja na hilo kuweni mabalozi wa kulinda rasilimali mbalimbali zinazotumika katika utekelezaji wa miradi katika maeneo yenu Ili kuhakikisha zinakamilisha kazi lakini miundombinu hiyo inufaishe wananchi " amesema.
Awali akitoa makadirio hayo, Afisa Mipango na bajeti katika halmashauri ya Arusha DC Anna Urio amesema kuwa katika bajeti hiyo, wamezingatia kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, kukarabati shule nne kongwe, kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisongo, na dampo la Bwawani.
"Pia tunataka msimu huu tuanze kuibua miradi ya hewa ya ukaa (carbon credits), tifanye upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa hotel ya nyota tatu katika eneo la karibu na mradi wa uwanja wa mashindano ya Afcon" amesema.
Amesema kuwa mafanikio hayo yote yatapelekea halmashauri yao kuongeza mapato, kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi lakini pia usafi na usalama wa mazingira na kuchangamkia fursa ya soko la utalii linaloonyesha kuchangamka Mkoani Arusha.
![]() |
Nae mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Sulemani Msumi amesema kuwa ukusanyaji mapato katika Ofisi yake imeendelea kuimarika mara dufu.
Amesema msimu wa mwaka 2022/2023 walikusanya sh 4.6 Bilioni, huku mwaka 2023/2024 walikusanya sh5.4bilioni na mwaka 2024/2025 wamekusanya 6.9 kwenye makadirio ya kukusanya sh7.2 Bilioni.
Mwisho....