Arusha.Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wamesema kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya dawa za kulevya na matatizo ya afya ya akili inayoweza kusababisha wanafunzi kufeli darasani.
Kutokana na hilo, wamewashauri walimu na wazazi kutoa taarifa haraka za wahalifu wa dawa hizo kupitia namba ya simu ya bure ya 119.
Hayo yameelezwa na afisa Elimu kutoka DCEA Kanda ya kaskazini Shaban Miraji kwenye semina ya mbinu za kuwaepusha wanafunzi na tatizo la dawa za kulevya.
Semina hiyo iliyoshirikisha viongozi 58 wa matawi ya Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Arusha imetolewa jana katika Ukumbi wa Ofisi za Chama hiko Mkoani Arusha.
Aidha Miraji amesema kuwa matumizi ya dawa za kulevya kwa wanafunzi inaweza kupelekea kupata magonjwa ya akili na kufeli darasani.
"Hivyo Ili kumuokoa mwanafunzi wako inafaa umuepushe na matumizi hayo kwa kutoa taarifa haraka kwenye vyombo vya Ulinzi na usalama lakini pia kwa Mamlaka Ili aanze kusaidiwa kuachana nazo" amesema.
Pia aliwahamasisha kushirikiana na Mamlaka katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa hizo mitaani Ili kuokoa jamii nzima.
Mwisho