Arusha. Serikali imeipongeza benki ya NMB kwa kuwa msaada mkubwa kwa walimu nchini hasa katika utatuzi wa changamoto zao mbalimbali za kifedha.
Pongezi hizo zimetolewa Leo julai 14,2025 na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Karatu Juma Hokororo, kwenye kongamano kubwa la elimu ya kifedha iliyotolewa na maofisa wa benki ya NMB kwa walimu zaidi ya 220 kutoka shule mbalimbali za wilaya ya Karatu.
Hokororo amesema kuwa benki ya NMB imekuwa taasisi muhimu ya kifedha hapa nchini ambayo mbali na kusaidia serikali katika miundombinu mbalimbali lakini imekuwa msaada mkubwa kwa walimu kuwapatia masuluhisho ya kifedha ikiwemo mikopo.
Amesema kuwa walimu wengi nchini wamekuwa waathirika wakubwa wa mikopo umiza ambayo inatolewa na taasisi zisizo rasmi nchini kitendo kinachoshusha kiwango Chao za weledi kazini lakini pia kukumbwa na msongo wa mawazo.
"Wako waliotambua fursa ya mikopo ya NMB mapema na imekuwa ikiwasaidia kuinuka kiuchumi siku hadi siku, tofauti na wale wanaokimbilia mikopo umiza ambao wanadidimia Kila kukicha kutokana na masharti magumu ikiwemo riba kubwa" amesema Hokororo.
Amewataka NMB kuhakikisha elimu hiyo inasambazwa hadi kwa walimu walioko vijijini ili waweze kunufaika na elimu ya kifedha, uwekezaji na maandalizi ya kustaafu huku akiahidi ushirikiano wa kiserikali kufanikisha hilo.pppp
Mbali na hilo amewataka walimu kuepuka mikopo yenye masharti ya kuwadhalilisha na kushusha heshima ya taaluma yao ikiwemo inayotaka dhamana ya kadi ya benki wanayotumia kulipwa nazo mishahara.
"Mikopo ya hiyo wala haiwezi kuwasaidia kiuchumi zaidi inawadidimiza kwa kuwafilisi mnaposhindwa kulipa, hivyo kuanzia sasa hivi anzeni kuzingatia taasisi zenye heshima na hadhi kama NMB ambayo hata serikali inaitambua"
Meneja mwandamizi wa idara ya wateja binafsi kutoka NMB makao makuu, Ally Ngingite amesema lengo la kongamano hilo ni kuwapa walimu elimu ya kifedha, uwekezaji na maandalizi ya kustaafu kwa uchumi endelevu.
Amesema katika kongamano hilo zaidi ya walimu 220 kutoka shule mbalimbali Wilayani Karatu iliyoko Mkoani Arusha wamehudhuria ambao watakwenda kuwa mabalozi wa wengine.
"Elimu hii iko chini ya mpango wa 'mwalimu Spesho' unaotekelezwa na benki ya NMB kwa miaka 10 sasa kwa ajili ya kuwasaidia walimu katika nidhamu ya matumizi ya kifedha na fursa za uwekezaji kwa ajili ya ustawi wa uchumi wao na taifa kwa ujumla".
Amesema Lengo ni kuhakikisha walimu hawateseki tena na masuluhisho ya kifedha hasa uwekezaji isiyo na faida na na mikopo kausha damu.
Amesema kuwa kwa miaka 10 tangu kuanzishwa kwa mpango huo zaidi ya walimu 120,000 wamefikiwa.
"Ndani ya kongamano hili, pia tunawapa walimu elimu ya jinsi ya kujiandaa kustaafu kwa uchumi endelevu lakini pia maswala ya afya ya akili.
Nae Meneja wa NMB wilaya ya Karatu, Edgar Ninga, amesema kuwa elimu hiyo pia inawasaidia walimu kujua masuluhisho yao ya kifedha za kidigitali zinazotolewa na taasisi hiyo ili waweze kujihudumia mkononi bila ya kufuata Ofisi.
Mmoja wa walimu kwenye kongamano hilo, Matilda Mathiasi kutoka shule ya Karatu Sekondari amesema kuwa elimu hiyo ni muhimu kwao na itawasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kifedha wanazopitia walimu nchini.
Mwisho