Rostam Azizi ataka uwekezaji zaidi katika vyombo vya habari nchini

 

Mfanyabiashara Rostam Azizi 

Bertha Mollel 

Arusha.  Mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Azizi amezitaka sekta binafsi, wanahabari na asasi za kiraia kufanya uwekezaji zaidi katika vyombo vya habari hasa ujenzi wa majukwaa mapya ya kidijitali yenye uwezo wa kushindana.

 Amesema uwekezaji huo utasaidia nchi kukabiliana na taarifa za upotoshaji kwani itaeneza ukweli kwa mvuto, ubunifu, na weledi kwa kutumia utu na muktadha halisi wa Kitanzania.

Rostam aliyewakilishwa na mwandishi mwandamizi nchini Absolum Kibanda ameyasema hayo kwenye jukwaa la pili la mabaraza ya habari Afrika unaoendelea jijini Arusha wenye kauli mbiu “Uboreshaji wa sheria za usimamizi wa vyombo vya habari na mawasiliano ni msingi wa weledi wa uandishi wa habari Afrika” 

Amesema maudhui mengi mabaya yanayoongoza mijadala kuhusu Tanzania hayatoki ndani ya nchi bali  yanazalishwa na kusambazwa na watu wa nje wasioguswa na sheria, mila, wala misingi ya jamii za hapa nchini.

“Watu hawa mara nyingi hawana hisa katika amani yetu, hawana uwekezaji katika maendeleo yetu, na hawawajibiki kwa madhara ya maneno yao, ndio maana tunapaswa kuchukua hatua ya kuiwezesha Tanzania kumiliki na kuendesha majukwaa ya kisasa, yanayoweza kushindana katika uwanja wa kidijitali kwa kutumia ukweli, utu, ubunifu, na muktadha halisi wa Kitanzania”amesema na kuongeza;

“Tunahitaji kuwajengea uwezo vijana wetu wa habari za kidijitali, wabunifu wa mitandao, wataalamu wa data na artificial intelligence (AI)  ili waweze kutoa habari na kusimulia simulizi ya taifa letu kwa macho yetu, kwa sauti yetu, na kwa misingi yetu”.

Rostam ambae ni mwakilishi wa wamiliki wa vyombo binafsi, amesema kuwa kufanikisha hilo si suala la usalama wa taifa pekee bali pia ni la uhuru wa kifikra na uhuru wa kitaifa ambayo ni msingi inayopaswa kulindwa na wale ambao wana mizizi kwenye ardhi ya Tanzania.

Mkutano huo wa siku tatu wenye lengo la kujadili kustakabali wa ustawi wa vyombo vya habari katika zama hizi za ukuaji wa teknolojia, umeandaliwa na mtandao wa mabaraza huru  ya habari Afrika (NIMCA)kwa kushirikiana baraza la habari Tanzania (MCT).

Mwenyekiti  wa NIMCA, Ernest Sungura alisema mkutano huo wa pili Afrika kufanyika unakutanisha zaidi ya mabaraza ya habari 19 ya vyombo vya habari Afrika  na nje ambapo pamoja na mambo mengine wanatarajia kuweka mikakati na mbinu mbadala wa kurejesha nguvu ya kiuchumi kwa vyombo vya habari ambayo inapotea kwa haraka kutokana na mabadliko ya kiteknolojia na kupunguza uhuru wake katika kujieleza na unaozingatia maadili na weledi

“Changamoto  zinazokumba vyombo vya habari Afrika inahitaji nguvu na sauti moja katika kutafuta suluhu ya changamoto hizo, ikiwemo kukuza uchumi , kulinda uhuru,  ili viendelee kutekeleza wajibu wao wa kufahamisha, kufichua na kuelimisha na kuburudisha kwa kuzingatia maadili na weledi”

Mbali na hilo sungura amesema wanatarajia kujifunza namna vyombo vya habari katika mataifa mengine wanavyosimamia tasnia ya habari na kuhakikisha waandishi wa habari na wahariri wanatekeleza wajibu wao wa msingi kwa kuzingatia weledi na madili.

“Pia tunatarajia kuboresha mashirikiano katika kuboresha sheria ya vyombo vya habari na mawasiliano ambayo tunaamini ndio msingi wa weledi wa aandishi wa habari duniani”.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!