Waziri Ndumbaro aweka wazi kilichoiondoa Tanzania kwenye itifaki ya mahakama ya AfCHPR,



Arusha. 

Serikali ya Tanzania imesema Iko tiyari kukaa meza moja kwa mazungumzo na uongozi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) ili kushughulikia changamoto zilizopelekea kujiondoa kwenye itifaki iliyoanzisha Mahakama hiyo.

Tanzania ilikuwa moja ya nchi nane wanachama wa Afrika zilizotiasaini tamko la Kifungu cha 34(6) la kuruhusu watu binafsi na mashirika binafsi 'NGO' kuwasilisha kesi moja kwa moja katika mahakama ya ACHPR kabla ya kujiondoa baadae.

Dk Ndumbaro amesema, Tanzania ilikumbwa na changamoto katika kutekeleza baadhi ya maamuzi ya Mahakama hiyo, hasa katika kesi zinazohusisha wafungwa waliopatikana na hatia kwa makosa makubwa kama ubakaji na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Dk Ndumbaro amesema hayo Leo january 30,2025 jijini Arusha wakati akifungua mjadala katika jukwaa la wadau wa haki na mahakama ya Afrika kuelekea kikao cha kwanza cha mahakama ya Afrika inayotarajia kuanza Desemba 3,2025.

"Kwa mfano moja ya hukumu, Mahakama iliagiza Tanzania iwalipe fidia wafungwa waliokosa msaada wa kisheria kiasi cha Sh300,000 za kitanzania ambazo ni takriban Dola za Kimarekani 125,  Serikali iliona ugumu katika kutekeleza maamuzi kama haya kwa sababu jamii haikubali kufidia watu waliopatikana na hatia ya makosa makubwa kisheria," alisema Dk. Ndumbaro.

Aliongeza kuwa kujiondoa kwa Tanzania kwenye Kifungu cha 34(6) cha Itifaki hakumaanishi kukataa Mahakama hiyo moja kwa moja, bali ni mwitikio wa changamoto za kisheria na sera zinazokinzana kati ya maamuzi ya Mahakama na mfumo wa sheria wa Tanzania.

"Hili linapaswa kuwa mwito wa tafakuri kwa nini mataifa mengi yanasita kujitolea kikamilifu kwa Mahakama hii je kikwazo ni nini" amesema 

Amesema Kati ya nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika, ni nchi 34 pekee zilizoridhia itifaki ya kuanzisha Mahakama hii. Kabla ya Tanzania kujiondoa, ni mataifa manane tu yaliyokuwa yamesaini tamko la Kifungu cha 34(6) linaloruhusu watu binafsi na NGO kuwasilisha kesi moja kwa moja. Sasa, baada ya Tanzania kujiondoa, ni mataifa saba pekee yaliyobaki," alibainisha.

Alisema pia kuwa wasiwasi juu ya kuruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) kuwasilisha kesi moja kwa moja Mahakamani si jambo linalohusu Tanzania pekee, bali ni suala linalozua mashaka miongoni mwa mataifa mengi ya Afrika, likionyesha hitaji la mjadala mpana kuhusu muundo na utendaji wa Mahakama hiyo.

Licha ya changamoto hizi, Dk. Ndumbaro alisisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuunga mkono Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, hususan dira yake ya "Afrika yenye Utawala Bora, Demokrasia, Heshima kwa Haki za Binadamu, Haki na Utawala wa Sheria."

Pia amesema kama Tanzania wako na utayari wa kurejea kwenye mazungumzo na Mahakama ili kupata suluhisho linalofaa kwa Tanzania kurejea kwenye mfumo huo.

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Muungano wa Mahakama ya Afrika na Mkurugenzi wa Umoja wa Wanasheria wa Pan-Afrika (PALU), Donald Deya amesema mjadala huo una umuhimu katika kushughulikia changamoto za Mahakama, athari zake, na mageuzi yanayoweza kufanikisha malengo yake ya awali.

"Mjadala huu wa wadau unaleta pamoja wawakilishi kutoka Afrika nzima ili kujadili kabla ya kuanza kwa Kikao cha Kwanza cha Kisheria cha ACHPR kwa mwaka huu, kinachotarajiwa kuanza tarehe 3 Februari 2025," alisema.

Deya pia alieleza kuwa migogoro na vita katika mataifa mengi ya Afrika inaonyesha umuhimu wa Mahakama hiyo katika kusuluhisha migogoro kwa njia ya amani.

"Tumejumuika hapa kutathmini iwapo Mahakama hii inawatumikia watu ipasavyo. Mataifa mengi ya Afrika kwa sasa yanakumbwa na migogoro, lakini badala ya kutegemea mifumo ya kisheria, migogoro hiyo inatatuliwa kwa njia za vita. Hii ni ishara wazi kuwa kuna mapungufu ndani ya Mahakama yanayohitaji kushughulikiwa," alisema.

Aidha, alisisitiza hitaji la kuimarisha utetezi wa Mahakama, si tu ndani ya Afrika bali pia kimataifa, ili kuongeza ufanisi wake katika kukuza amani, maendeleo ya kiuchumi, afya, na biashara barani Afrika.

Nae Naibu Msajili wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Grace Kakai amesema wameandaa jukwaa hilo Ili kupata njia za kuimarisha mfumo wa haki za binadamu wa Afrika.

"Kupitia mazungumzo yanayoendelea, wadau tunatarajia kufungua njia ya kuwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliyo jumuishi zaidi, yenye ufanisi, na inayoaminika" amesema.

Mwisho..

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!