Wataalamu 700 wa rasilimaliwatu na utawala kukutana Arusha kujadili maboresho ya utendaji kazi kupitia teknolojia

 




Arusha 

Zaidi ya wataalamu 700 wa usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala katika sekta ya umma wanatarajiwa kukutana jijini Arusha kujadili mwelekeo mpya wa utendaji kazi unaolenga kuendana na kasi ya mageuzi ya teknolojia.

Wataalamu hao wanatarajiwa kushiriki katika Mkutano mkuu wa kwanza wa Mwaka wa Jumuiya za Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala katika Utumishi wa Umma.

 Mkutano huo wa TAPA-HR, utaanza Julai 22 hadi 25, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Mkutano huo umeandaliwa na Ofisi ya Rais- Utumishi na Utawala Bora, chini ya kaulimbiu "Mwelekeo mpya wa nafasi ya wataalamu wa usimamizi wa rasilimaliwatu na Utawala: Kusukuma Mabadiliko, kuendana na mageuzi ya teknolojia kwa ajili ya kuboresha huduma katika utumishi wa umma.”

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 18, 2025 jijini Arusha, Mwenyekiti wa TAPA-HR, Grace Meshy, alisema mkutano huo unaofanyika kwa mara ya kwanza nchini, utafunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene.

 Meshy alisema kuwa mkutano huo ni sehemu muhimu ya mkakati wa kujiandaa kukabiliana na mazingira ya utendaji yanayobadilika kwa kasi, hasa katika nyanja za kidijitali, ili kuongeza ufanisi katika taasisi za umma.

“Kasi ya mabadiliko ya teknolojia inaonyesha wazi kuwa kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu wa utawala na rasilimaliwatu wenye uwezo wa kuendana na mabadiliko hayo ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema  Meshy.

Alibainisha kuwa mkutano huo utakuwa jukwaa la kipekee kwa wataalamu hao kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uwezo wao wa kitaaluma ili kuleta mageuzi chanya katika taasisi za umma.

Kwa mujibu wa Meshy, mkutano huo pia unatarajiwa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha weledi, maadili na mifumo ya kiutendaji miongoni mwa wataalamu wa kada ya rasilimaliwatu na utawala nchini.

Naye Katibu wa TAPA-HR, Prisca Lwangili, alisema mkutano huo utahusisha mada mbalimbali zenye lengo la kuboresha mbinu bora za kiutawala, kuimarisha uongozi, matumizi ya TEHAMA, na kukuza uwajibikaji katika sekta ya umma.

“Tunaomba waajiri kutoka wizara, mamlaka za serikali za mitaa, wakala wa serikali, mashirika ya umma, vyuo vikuu na taasisi nyingine za umma kuhakikisha wanawawezesha wataalamu wao kushiriki katika mkutano huu, kwani ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa maendeleo ya rasilimaliwatu na utawala bora,” alisema.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!