Kihongosi ataja misingi ya Arusha anayoitaka


 

Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenani Kihongosi ameongoza mamia ya wakazi wa Arusha kufanya mazoezi huku akitaka Upendo, Umoja na Mshkamano kuwa misingi na nguzo ya Mkoa wake.

“Arusha tukatae majungu, umbeya na unafki pia watu wanaogawanyisha watu, nataka tushikamane ,tuishi kwa upendo mkubwa kwani maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana hivyo huna sababu ya kumchukia yoyote wala kumuumiza yoyote” amesema

Kihongozi amesema hayo baada ya kufanya mazoezi leo jumamosi Julai 19, 2025 katika uzinduzi wa klabu ya mazoezi jijini Arusha iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya mkuu wa Mkoa.

Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wakazi wa Arusha kwa kuamua kufanya mazoezi ambapo amewataka maofisa wa ofisi yake akiwemo mkuu wa polisi Wilaya kuhakikisha kila jumamosi mazoezi yanafanyika na kushirikisha wakazi wote wa Arusha wanaopenda kufanya hivyo.

“Nataka kila jumamosi tufanye mazoezi hapa kwani mazoezi ni afya yako mwenyewe kwa kuondoa magojwa yasiyo ya kuambukiza hivyo twenden tujengeni Arusha nzuri” amesema.

Mbali na hilo Kenani amewataka wakazi wa Arusha  kushiriki vema uchaguzi usio na vurugu huku wakichagua viongozi wenye nia ya kuwatumikia.

“Hapa Arusha tunahitaji amani, hatuhitaji vurugu hivyo niwaombe vijana wenzangu asiwepo mtu yoyote akakuambia uende ukaandamane ukafanye vurugu na ukafanye fujo kwani mchuma janga atakula na wa kwao na wewe ukichuma utakula na wa kwenu sio huyo aliyekutuma” amesema

 

Wadhamini wakuu kutoka Benki ya NMB, wamesema kuwa wameamua kudhamini mazoezi hayo kutokana na kutambua umuhimu wa afya njema hasa katika kuongeza mapato ya Mkoa na uchumi kwa ujumla.

Akizungumza katika mazoezi hayo, Meneja mwandamzi wa idara ya wateja binafsi kutoka NMB makao makuu Ally Ngingite amesema kuwa wataendelea kusapoti michezo na mazoezi yote yatakayofanyika Arusha kwani hiyo pia itaongeza wateja kwao.

“Tunampongeza sana Mkuu wetu wa Mkoa kwa kutuletea ratiba hii nzuri ya mazoezi ambayo itafanyika kila jumamosi hapa Arusha na sisi tuko bega kwa bega na ninyi kihakikisha yanafanikiwa”

Pia amesema kuwa wataendelea kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi lakini pia masuluhisho kifedha yanayopatikana NMB ili kuwasaidia wananchi kunufaika kiuchumi katika biashara na kazi zao na familia zao.

“Kubwa tunalenga kuwaokoa na mikopo umiza, lakini wajue kuweka vipaumbele kulingana na kipato wanachokipata na bajeti ili kutumia kipato chao katika kuwekeza katika shughuli mbalimbali “

“Katika Elimu hii pia tunajumuisha mafunzo ya afya ya akili na zaidi kuwaelimisha watumishi wa kada mbalimbali juu ya maandalizi ya kustaafu” amesema.

Nae mmoja wa wana mazoezi Pamella Mollel amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kuanzisha jambo hilo zuri na kusema itasaidia pia kukuza uchumi wa Mkoa

“Hakuna jambo zuri kama kufanya mazoezi kwa afya, na afya ndio msingi wa kufanya kazi na kuingiza kipato na kuondokana na utegemezi hivyo Arusha inakwenda kuchangamka tena”

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wakazi wa Arusha kuhakikisha kunahudhuria mazoezi hayo kila jumamosi kwa ajili ya afya zao lakini pia kutengeneza mtandao wa kibiashara na wadau wengine.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!