Wananchi Sinoni walia na serikali kusuakusua ujenzi wa barabara ya Engosheraton


Arusha. 
Wananchi wa kata ya sinoni jijini Arusha wameonyesha wasiwasi wa kutokumalizika kwa barabara ya Engosheraton iliyoko ndani ya Jiji la Arusha kutokana na ujenzi wake kusimama kwa mda mrefu huku mkandarasi akihamisha vifaa vya kazi.

Kutokana na hilo, wananchi hao wameiomba serikali iongeze nguvu katika usimamizi wa kazi hiyo kuhakikisha ujenzi unaisha kwa wakati Ili kupunguza mateso wanayoyapata kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Wananchi hao wameyasema hayo jana kwenye ziara ya M'bunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo alipotembelea mwenendo wa ujenzi wa barabara ya Engosheraton yenye urefu wa kilomita 4.8 iliyoanza kujengwa November 2023 ikitarajia kukamilika February 2025 kwa gharama ya Sh4.6 Bilioni.

Mmoja wa wananchi hao Shiwa Madulu amesema kuwa tangu kuanza kwa ujenzi huo imeharibu miundombinu muhimu ikiwemo ya maji safi na taka na kupelekea wao kuteseka bila maji katika kipindi chote .

"Mabomba yalikatwa katwa na kukatisha Maji hivyo tumekuwa tukifuata umbali mrefu kwa wenzetu wa barabara ya pili upande wa uswahilini mbaya zaidi mifumo ya maji taka pia imeharibiwa vibaya na kusababisha chemba za maji taka kubaki wazi na kutoa harufu Kali na kuleta hatari kwa watumiaji wa barabara lakini zaidi watoto wanaocheza pembezoni" amesema na kuongeza;

"Tuliamua kuvumilia tukiona ujenzi unaendelea shida itaisha, lakini sasa ni miezi miwili hatuoni chochote na mbaya zaidi mitambo yote imehamishwa bila kujulishwa chochote huku barabara ikiachwa na mabonde na milima na lindi la vumbi" amesema.

Sophia Simba alisema kuwa barabara hiyo iliyoanza kuchimbwa ilisimama kipindi cha mvua na kuleta adha kubwa kwa watumiaji wake kutokana na tope kubwa iliyosababishwa na udongo uliochimbwa.

"Wanawake tuliteseka na tope, watoto wetu waliteseka na utelezi ya milima na mabonde kipindi cha mvua,  hiyo haitoshi leo tunateseka na vumbi kali inayopepea na kimbuka kikali na kuzama kwenye nyumba na biashara zetu na wengine biashara ya mihogo, samaki na mboga mboga imekuwa ngumu kwa kuchafuka na vumbi"amesema.

Akizungumzia swala hilo, mkandarasi wa barabara hiyo, Wu Zhoufa kutoka kampuni ya ujenzi ya Jiangxi-Geo engineering group ltd amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo imesusua kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kwa mfululizo kutoka mwezi Octoba mwaka hadi Desemba mwaka jana.

Amesema kazi hiyo ya miezi 15 wameshatumia asilimia 86 ya mda (miezi 13) huku kazi ikiwa imekamilika kwa asilimia 60 ambapo anatarajia hadi Februar 28,2025 atakamilisha kazi hiyo.

"Changamoto kubwa ni mvua ndio ilikwamisha na kuhamishwa kwa vifaa tuliogopa ingeharibika hapa kutokana na mvua kubwa na udongo kuzidi kutitia lakini kuanzia sasa tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunakamilisha ndani ya mda na kukabidhi" amesema.

Akizungumza katika barabara hiyo, Gambo amesema kuwa hofu ya wananchi hao inazidi kutokana na kuhamishwa vifaa vya kazi hivyo kuwataka wakala wa barabara vijijini (Tarura) kuzidisha nguvu ya usimamizi katika barabara hiyo kuhakikisha ujenzi unaisha ndani ya wakazi.

"Kuna shida hapa tusidanganyane eti ndani ya miezi 13 mtu amejenga asilimia 60 pekee halafu ndani ya miezi miwili akamilishe asilimia 40 iliyobaki, huo ni uongo maana hata vifaa havipo kazini vikiendelea na kazi zaidi ya wananchi kuteseka" amesema Gambo na kuongeza;

"Tarura Kuna mahali mlizembea kwenye usimamizi wa hii kazi hadi leo iko hivi sasa niwaambie ongezeni usimamizi maana serikali imeshatoa hela ya kutosha ya mradi huu, na kama mkandarasi asipomaliza kazi kwa mda apewe adhabu na mimi nitasemea hili bungeni Ili wakandarasi wababaishaji wasipewe kazi tena Arusha "amesema.

Gambo pia amesema kuwa ataendelea kutembelea, kukagua na kusisitiza miradi ya maendeleo itekelezwe kwa wakati na kwa kiwango chenye ubora, na penye mapungufu ataendelea kusema hadharani bila kujali watu wengine watasema nini.

"Tutaendelea kusema hadharani changamoto za Wananchi ili zipate utatuzi na kamwe hatutasemea chumbani kama wengine wanavyotaka"amesema Gambo na kuongeza;

"Kusema kwangu nataka watu wapate Suluhu ya mateso yao haijalishi nani anataka nani hataki au nani atafurahi na nani atachukia maana Mimi ndio sauti ya wananchi hawa" amesema Gambo.


Kwa upande wake mhandisi kutoka Tarura, Vicky Chisoma amesema kuwa Bado kazi hiyo Iko ndani ya mda hivyo watasubiri kuona mwisho wake.

"Uzuri mkandarasi amehaidi atamaliza kazi kwa wakati akidai kazi iliyokuwepo chini ilikuwa kubwa zaidi ya iliyobaki sasa ya kuweka lami pekee, hivyo tunasubiri kuona hitimisho" amesema.

Mwisho.
Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!