Bertha Mollel
Arusha. Naibu waziri Mkuu na Waziri wa nishati Dk Doto Biteko amewataka Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini (PSPTB) kuendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu wataalam wa maswala ya Ugavi wanaotekeleza majukumu yao chini ya kiwango cha taaluma au kimaadili.
Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuilinda taaluma hiyo muhimu katika kujenga uchumi wa nchi ambayo inatumia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya serikali.
Mbali na hilo amewaelekeza waajiri wote nchini, ikiwemo Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kuhakikisha kazi za ununuzi na ugavi zinafanywa na wataalamu wenye sifa na waliosajiliwa na PSPTB.
Dk Biteko ameyasema hayo kwenye kongamano la 15 la wataalam wa ununuzi na ugavi Linakofanyika kwa siku nne Mkoani Arusha.
"Nimetaarifiwa kuwa, Bodi imechukua hatua kwa Wataalamu 14 walioonekana kutekeleza majukumu yao chini ya kiwango cha taaluma yao kama ilivyobainishwa na taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA)"
"Lakini pia nimesikitika kusikia kuwa wapo baadhi ya Watumishi ambao wamebainika kufanya kazi pasipo na sifa stahiki na bila kusajiliwa na Bodi kama ilivyo takwa la Kifungu cha 11 cha Sheria ya PSPTB".
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PSPTB, Benezeth Ruta, amesema changamoto kubwa kwa sasa ni maslahi madogo wanayoyapata wanataaluma katika mishahara yao tofauti na taaluma zingine.
"Changamoto kubwa katika taaluma hii ni maslahi madogo kwa wataalamu hawa hasa wanaohitimu cheti cha kitaaluma cha CPSP, tulishawasilisha kwa wizara yetu tunasubiri utekelezaji "
Katika hilo Biteko alisema mchango wa Wataalamu hao ni muhimu hivyo uthaminiwe ili wataalamu hao waweze kufanya kazi bila vishawishi na kwa kufuata maadili.
" Nikutake Waziri mlifuatilie suala hili ili lifikie mwisho kwa maslahi ya wataalamu hawa, na kufikia mwaka ujao wa fedha, wataalamu hawa wapate tabasamu la Mama yetu, Mheshimiwa Dk Samia Suluhu uluhu Hassan" amesema Dk Biteko
Nae naibu waziri wa fedha Hamad Chande amewataka wataalam hao kuzingatia taaluma na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ukizingatia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya serikali wanapangia matumizi wao.
Kwa niaba ya wadhamini wakuu wa mkutano huo, Meneja Mkuu wa masoko kutoka Bulk distributors ltd Juzar Sachak alisema kuwa wameamua kudhamini kongamano hilo kwa kutambua umuhimu wa sekta ya manunuzi nchini.
"Ni muhimu kwa uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi hasa katika kudhibiti Rushwa, kuharakisha bidhaa katika manunuzi na kuzingatia ubora wa bidhaa inayotumika kutekeleza miradi hiyo ndio maana Leo tupo hapa kushirikiana nao" amesema Suchak.