Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza mjadala wa wataalamu wa magonjwa ya mifugo juu ya kukabiliana nazo katika kuongeza uzalishaji wa bidhaa za wanyama hao nchini kwa utoleshelevu wa mahitaji lakini pia kuongeza pato la Taifa.
Kwa mujibu wa mtandao wa kituo cha uwekezaji nchini (TIC), mahitaji ya nyama nchini ni tani milioni 290 huku uzalishaji ukiwa ni asilimia 30 tu na sababu kubwa ikitajwa ni magongwa yanayowakumba mifugo
Hata hivyo Mahitaji ya nyama ya ndani yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 166 kutoka tani milioni 290 hadi tani milioni 480 ifikapo mwaka 2030 kutokana na ongezeko la idadi ya watu.
Katika kukabiliana na hilo, Wataalamu wa magonjwa ya Mifugo nchini na wale wa nchi za jumuiya ya madola wanatarajia kujifungia kwa siku tatu jijini Arusha kwenye kongamano la 42 la wanachama wa Kitaaluma cha Kisayansi cha madaktari wa Mifugo Tanzania{TVA} kuazia kesho Desemba 3 hadi 5, 2024 kwa ajili ya kujadili suluhu ya magonjwa ya mifugo.
![]() |
Mwenyekiti wa TVA, Profesa Esron
Karimuribo |
Akizungumza na waandishi wa habari leo desemba 2,2024 mwenyekiti wa TVA, Profesa Esron Karimuribo amesema kuwa kauli mbiu ya Kongamano hilo ni ‘Tokomeza magonjwa wa mifugo ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuimarisha biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi’.
“Tunataka kuongeza tija ya mazao ya mifugo nchini katika kuzuia magonjwa mapya yasiingie lakini hata yaliyopo kukabiliana nayo yasilete madhara kwa manufaa ya nchi kiutoshelevu wa bidhaa za wanyama lakini pia kuongeza pato la Taifa kuuza nje ya nchi”amesema.
Amesema kuwa kongamano hilo litakalokuwa na washiriki zaidi ya 2000 pia watajadiliana na kubadilishana uzoefu na wataalamu wengine wa magonjwa ya mifugo kutoka nchi za jumuiya ya Madola juu namna ya haraka ya kukabiliana na magonjwa ya wanyama kwenda kwa binadamu.
“Magonjwa yote ya milipuko na mengine kama Kimeta, Homa ya nyani na kichaa cha mbwa yamekuwa yanaathiri wanyama lakini pia yanawakumba binadamu hivyo tunatarajia kupata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wenzetu kukabiliana nayo” amesema.
Kwa upande wake Katibu msaidizi wa TVA amesema katika kongamano hilo watakuwa na maonyesho mbalimbali ya wataalamu wa wazalishaji wa chanjo na dawa za wanyama ili kupunguza pia gharama kwa serikali kuagiza bidhaa hizo nje lakini pia kuokoa maisha ya wanyama wanaokufa kutokana na kukosa chanjo na dawa kwa wakati.
“Lengo ni kuonyesha kuwa Tanzania tunaweza kuwekeza kwenye vitu vyetu wenyewe lakini pia kuhamasisha wadau wa sekta binafsi kushirikiana na serikali katika uwekezaji wa viwanda vya uzalishaji wa chanjo na dawa za mifugo”.
Nae mtafiti wa magonjwa ya wanyama kutoka taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) Profesa Gabriel Shirima amesema kuwa upo umuhimu mkubwa wa utafiti wa mara kwa mara juu ya maendeleo ya wanyama nchini ili kubaini hatari ya magonjwa yajayo lakini namna ya udhibiti wake mapema.
“Tutakapokutana na wenzetu tutabadilishana pia tafiti mbalimbali zilizofanyika juu ya magonjwa ya wanyama na namna ya kukabiliana nazo ikiwemo hatari na udhibit wa mapema” amesema.
Mwisho