Kitanzi kipya kwa wazazi wanaohujumu watoto wenye ulemavu

 


Arusha.

 Serikali imetangaza kiama kwa wazazi na walezi wanaowaficha watoto wao wenye ulemavu na kusababisha kukosa haki yao ya kupata Elimu. 

Mbali na hilo, pia itawachukulia hatua za kinidhamu viongozi watakaibainika kuwa kikwazo cha utekelezaji wa majukumu ya ufundishaji kwa walimu wenye mahitaji maalumu au wanaowafundisha wanafunzi wenye ulemavu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa katika shule maalumu ya Sekondari Patandi wilayani Arumeru Mkoani Arusha kwenye maadhimisho ya miaka 30 ya utekelezaji wa elimu Jumuishi.

Maadhimisho hayo ni utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa Salamanka uliosainiwa na serikali mwaka 1994 na kuanza kutumika rasmi mwaka 1997.



Waziri Mchengerwa amesema kuwa imewapa haki ya kisheria watoto wote kupata elimu Jumuishi bila kujali kasoro yoyote ya kimwili na kiakili.

Amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanatumia vyombo vyao vya ulinzi na usalama vema na vyombo vya taarifa vya ngazi ya mitaa na kata, kuhakikisha wanawabaini wazazi na walezi wanaowaficha watoto wenye ulemavu ili kuwapora haki yao ya kupata elimu.

“Serikali imekuwa ikitoa matamko, lakini pia kuandaa sera, mikakati na Sheria za utekelezaji wa Elimu Jumuishi lakini bado kuna watu wenye kufikiri kwamba mtoto mwenye changamoto hana haki ya kupata elimu” amesema Mchengerwa na kuogeza;

“Sasa nawaagiza, mkaweke utaratibu wa kufuatilia kila kona kwenye jamii zetu kuwabaini watu hao ili serikali iweze kuchukua hatua haraka za kisheria dhidi yao”amesema Mchengerwa.

Amesema, mbali na maboresho ya miundombinu lakini pia elimu na hamasa inayotolewa na serikali kwenye jamii, muamko wa wazazi na walezi kuwafichua watoto wenye mahitaji maalumu umeongeza idadi yao mashuleni.

“Hadi sasa idadi ya wanafunzi walioko katika ngazi mbalimbali za Elimu nchini imefikia 78,429 kwa mwaka 2024 kutoka 28482 kwa mwaka 2020"

" Kutokana na Ongezeko hilo serikali imetenga jumla ya shule 6088 za kuwapokea wanafunzi hao huku kati ya hizo 309 zikiwa na Mabweni”amesema Mchengerwa.



Mbali na hilo pia serikali imejenga shule mbili maalumu za mfano, sambamba na kujenga mabweni 172 kwa mfuko wa serikali kuu, pia vyumba 44 na matundu ya vyoo 132, ambapo Mchengerwa amesema ni kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa shule za msingi kote nchini.

“Pia imetolewa jumla ya Sh8.3 Bilioni kwa ajili ya kununua na kusambaza vifaa maalumu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika taasisi za elimu, hivyo hatutakuwa tiyari kuona juhudi hizi zinakwamishwa na wachache wanaoficha watoto wakati serikali inazidi kuboresha miundombinu ya kuwapatia elimu kila kukicha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu Maalumu Dk. Magreth Matonya kutoka wizara ya elimu sayansi na teknolojia, alisema maadhimisho hayo ya miaka 30, yametokana na  kuanza utekelezaji wa elimu jumuishi nchini ambapo Tanzania ilisaini mkataba wa kimataifa mwaka 1994.

"Maadhimisho haya yana malengo manne, kutangaza fursa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, kutangaza mafanikio, kutoa elimu ya uhamasishaji kwa wazazi wanaowaficha watoto na kutoa tathimini tulipo na tunapoelekea"amesema Dk Magreth.

 

Dkt Matonya alisema dhana ya elimu Jumuishi ni kuwaweka pamoja wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu waweze kusoma kwa kutegemeana na kusaidiana.

Alisema kwa sasa wanatumia zaidi ufundishaji wa matumizi ya teknolojia kwa wanafunzi ili waweze kuendana na mabadiliko ya mapinduzi ya nne ya viwanda kwa ajili ya hatma ya maisha yao badae hasa katika ajira.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!