TUICO watahadharisha wafanyakazi dhidi ya utitiri wa vyama

 

Mkuu wa Idara ya Sheria kutoka Tuico, Noel Nchimbi 

Arusha

 Chama cha Wafanyakazi,TUICO kimewataka wafanyakazi kuwa  makini na utitiri wa vyama vinavyowatembelea na kuwashawishi kujiunga.

Amesema lengo la umakini huo  ni ili kuepuka kutapeliwa, kuibiwa au hata taarifa zao kutumika vibaya kwa matumizi ya wizi au udanganyifu sehemu zingine kwa manufaa ya watu binafsi.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Sheria kutoka Tuico, Noel Nchimbi wakati akitoa semina kwa wafanyakazi wa idara ya maji jiji la Arusha (AUWSA) juu ya maswala ya kazi, wajibu na haki zao kazini na kwa muajiri.

Nchimbi amesema kuwa hivi karibuni kumeibuka na utitiri wa vyama vinavyojinasibu kutetea maslahi ya wafanyakazi wa kada mbalimbali huku baadhi yao wakiwasili katika ofisi za waajiri hasa za sekta binafsi na kuwashawishi wafanyakazi kujiunga nao.

“Nitoe Rai kwenu, pamoja na kuwa tumepewa uhuru wa kuchagua kujiunga na vyama, lakini tuwe makini nao wanapokuja kwanza asikuitie mkutano uchochoroni yaani nje ya ofisi unayofanyia kazi pia awe na kibali cha mwajiri, lakini jiridhishe na maswali kadhaa ikiwemo ofisi zao ziko ngapi na mikoa ipi, wana wanachama wangapi, lakini kubwa wana mikataba mingapi ya hali bora na piga simu mikoa husika aliyotaja uulize”.

“Lengo la kufanya hivi ni kuepuka utapeli, udanganyifu, wizi au matumizi ya taarifa zako utakazozijaza kujiunga kutumika vibaya na kukuhaibia sifa baadae, kwani kwa sasa kila kada au taaluma inajinasibu kuanzisha chama lakini nyingi ni kwa maslahi ya waanzilishi bila kuangalia wanachama wao” amesema Nchimbi.

Mbali na hilo amewataka waajiri kuchuja sera za watu wanaojitokea kwenye ofisi zao kutaka kukutana na wafanyakazi wao kwa ajili ya kuwashawishi kujiunga na vyama hivi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Nchimbi amesema kuwa lengo la kutoa Onyo hilo ni kwa sababu vilio vimekuwa vingi mitaani vya wafanyakazi kutapeliwa au kuibiwa fedha zao kwa madai ya kutoa kiingilio cha chama au kutoa hela za dhamana ili kupewa mikopo lakini haitekelezwi au inakuwa kandamizi.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafanyakazi Auwsa, Said Galambo amesema kuwa semina hiyo iliyohusisha wafanyakazi wa idara ya maji walio wanachama na wasio wanachama wa Tuico imesaidia kupanua ufahamu wao juu ya usalama, haki na wajibu wao kazini na kwa muajiri.

“Hakuna haki bila wajibu, hivyo tumeona kadri unavyotekeleza wajibu wako ndivyo na haki ilivyopatikana hivyo tunaomba mafunzo kama haya yaje mara kwa mara ili wafanyakazi waendelee kuelewa na kutekeleza majukumu yao.

“Pia waendelee kusaidia wenzetu waliorubuniwa kurudi kwenye vyama vya msingi” amesema Said.



Nae Halima Mwahu ameiomba Tuico kuhakikisha wanaendelea kupigania mazingira ya mwanamke anapokuwa kazini kupata stahiki zake hasa kipindi cha mimba, uzazi hadi kunyonyesha.

“Waendelee kutupigania maana kuna baadhi ya maeneo unaogopa hata kubeba mimba maana unaiweka kibarua chako hatarini cha kufukuzwa, lakini tukijifungua tupewe mda wa kunyonyesha watoto kwa kupunguziwa masaa ya kuingia kazini, hiyo itasaidia kutufanya huru na kazi lakini pia na jinsia zetu” amesema Halima.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!