![]() |
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa |
Arusha
Serikali sasa kuja sasa na mpango wa kutoa barua ya Utambulisho wa mkazi kidigitali kwa kutumia mfumo wa Anwani ya makazi (NaPA) ili kuepuka usumbufu kwa wananchi kufuata huduma hiyo kwenye ofisi za watendaji wa kata au mitaa.
Barua hiyo ya utambulisho ambayo hutolewa na watendaji wa kata au mitaa, huhitajika katika utambulisho wa maombi ya huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo maji, umeme, ajira za pamoja na ufadhili wa masomo.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa kwenye ufunguzi wa uhakiki wa taarifa za anwani za makazi Mkoa wa Arusha ulioanza kwa mafunzo ya siku mbili kwa watendaji na wenyeviti wa mitaa na kata.
Amesema kuwa utoaji wa barua hizo kidigitali utakaoanza baada ya zoezi la uhakiki wa anwani ya makazi ni kuwezesha mpango wa serikali wa kuhudumia wananchi kwa kutumia taarifa za anwani zao zitakazokuwepo kwenye mfumo.
“Hivyo baada ya zoezi hili la uhakiki kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti, wananchi hawatalazimika kwenda ofisini kwa mtendaji kupata huduma ya barua.
"Hivyo kuondokana na msongamano na kuongeza ufanisi katika ofisi za watendaji wetu lakini pia mianya ya udanganyifu na zaidi mwananchi ataepuka gharama na mda wake wa safari”amesema Mkapa.
Amesema, kwa sasa serikali imeanza kuwezesha watendaji wake mafunzo ya kutekeleza majukumu ya msingi ya mfumo wa anwani ya makazi ikiwemo kusajili anwani mpya, kuhuisha taarifa na kutoa barua za utambulisho wa wakazi kupitia mfumo wa anwani za makazi.
“Hatua hii inaongeza chachu ya kujenga misingi madhubuti ya utekelezaji na matumizi endelevu ya mfumo wa anwani ya makazi nchini kwa manufaa ya wananchi wenyewe katika maendeleo” amesema Mkapa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano kutoka Wizara ya habari, mawasiliano na Teknolojia ya habari, Mulembwa Munaku amesema kuwa utekelezaji wa NaPA unaofanyika kwa kuzingatia sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 ni makubaliano ya kikanda na kimataifa ya umoja wa Posta Afrika duniani katika kutambua mahali walipo wananchi wake.
“Lengo la utambuzi huo ni kuharakisha huduma za haraka zinazojitokeza kwa dharura ikiwemo huduma ya gari la wagonjwa, zima moto na uokoaji” amesema munaku.
Amesema kuwa katika kutambua hilo waliweza kufanya operesheni ya anwani ya makazi mwaka 2022 na kufanikiwa kukusanya taarifa za anwani milioni 12.3 nchi nzima huku kwa mkoa wa Arusha walipata zaidi anwani 442.
“Ni miaka miwili sasa imepita, na kutokana na changamoto za maendeleo, anwani hizi kuhama ndio maana serikali imeona umuhimu wa kuhuishwa kila wakati ili kuendelea kuwa na taarifa sahihi” amesema Munaku.
Kwa upade wake mwakilishi wa Tamisemi, Mhandisi Sutte Masula amesema kuwa zoezi hilo la uhakiki unatarajia kufanyika kwa siku 12 kuanzia Agosti14 hadi 24,2024, ikitanguliwa na semina ya kuwajengea uwezo watendaji wa kata na mitaa ambao ndio washiriki wakuu wa zoezi hilo kwa wananchi wao.
Nae Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, David Lyamongi amewataka watendaji hao kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa ikiwemo kurejesha nguzo na vibao vya barabara zilizoharibiwa ili kurahisha zoezi la anwani ya makazi kufanyika ndani ya mda uliopangwa.