Arusha
Watafiti wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini (TPHPA) wamesema kuwa wakulima na wafanyabishara wa pembejeo za kilimo wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na magonjwa ya Saratani na Mfumo wa Neva.
Hatari hiyo inasababishwa na sumu zitokanazo na viwatilifu wanavyotumia au wanavyouza kwa ajili ya kuulia wadudu, kutibu magonjwa ya mimea na hata kurutubisha mazao shambani bila kujikinga.
Rai hiyo imetolewa na Mtafiti wa kitengo cha upimaji na Udhibiti wa Sumu kwa binadamu kutoka TPHPA, Rose Kombo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Kombo amesema kuwa matumizi ya viuatilifu hayaepukiki kwa kilimo cha kisasa, hivyo kuwataka wakulima na wafanyabiashara wa pembejeo kuhudhuria kila baada ya siku 90 katika ofisi zao zilizoko mikoa yote Tanzania bara kwa ajili ya upimaji wa kiwango cha sumu walichovuta au kuingia mwilini kwa ajili ya kukabiliana na madhara makubwa wanayoweza kuyapata
“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wakulima na wafanyabiashara jinsi ya kujikinga unapotaka kutumia viwatilifu kwa kupiga kwenye mazao au unapopima kwa ajili ya biashara lakini baadhi yao wamekuwa hawafuati maelekezo hayo ya kujikinga vema bila kujua wanajiweka katika madhara makubwa” amesema Rose na kuongeza;
“Hivyo basi wakulima na wafanyabiashara wawe wanapima mara kwa mara kujua kiwango cha sumu kilichoingia mwilini ili kupata ushauri wa kukabiliana nao haraka bila kuleta madhara makubwa baadae”.
Amesema kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaofika kupima kila baada ya siku 90 na kukutwa na madhara, wamekuwa wakiwapatia ushauri wa kupunguza hadi kuondoa madhara ya sumu hizo ikiwemo kuwataka kunywa maji mengi, kufanya kazi za kutoka jasho au mazoezi ya mara kwa mara.
“Hizi sumu hazitolewi kwa dawa za hospitali kwani zinaweza kuongeza madhara zaidi, bali unatakiwa kukaa mbali na visababishi vya sumu hizo kwa mda si chini ya siku 90, lakini kunywa maji mengi ya kuleta haja ndogo mara kwa mara na kufanya kazi za kukutoa jasho jingi”
Amesema kuwa dalili za kuathiriwa au kuguswa na sumu ni kuumwa kichwa mara kwa mara, kuwashwa eneo lililoathirika, na kukohoa.
Amesema kuwa muathirika asipochukua hatua za haraka, sumu hizo kujijenga na kuleta madhara makubwa zaidi na huweza kusababisha maradhi ya kudumu kama Saratani ya Ngozi, kizazi lakini pia kuleta msongo wa mawazo, kuathiri mfumo na neva.
Kwa upande wake Mtaalamu wa kudhibiti visumbufu vya mimea kutoka TPHPA, Kenneth Nyakunga amesema kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kufanya tafiti mbalimbali za kudhitibiti visumbufu vya mimea lakini pia kutoa elimu kwa wakulima jinsi ya kutumia ili kuepuka madhara ya kiafya sambamba na mimea yao.
“Hizi sumu ni kwa ajili ya mimea hivyo haiwezi kuwa rafiki na binadamu ndio maana tunapowapelekea huwa tunawahimiza jinsi ya kupiga ilete matokeo, lakini pia vifaa vya kujikinga na namna ya kujikinga wasipate madhara, na wale wanaopata madhara kwa bahati mbaya wawahi kwenye ofisi zetu kupima na kupewa ushauri haraka” amesema Kenneth.