Hospital ya Seliani Lutheran kusogeza huduma za ugonjwa wa moyo Arusha

 

mkurugenzi wa hospitali ya Seliani iliyoko chini ya kanisa la Lutherani, (ALMC), Elisha Twisa (Kulia)akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dr. Mohammed Janabi 


Bertha Mollel ,Arusha 

Uongozi wa Hospitali ya Seliani iliyoko mkoani Arusha umeanza mikakati ya kufungua kitengo cha huduma za magonjwa ya moyo itakayohudumia wananchi wa kanda ya kaskazini.

Akizungumza na waandishi wa habari, mkurugenzi wa hospitali ya Seliani iliyoko chini ya kanisa la Lutherani, (ALMC), Elisha Twisa alisema kuwa wameamua kuanzisha kitengo hicho ili kusogeza huduma karibu kwa wagonjwa wa Arusha , Kilimanjaro na Manyara wanaokutwa na matatizo ya moyo  kuliko kuwapatia rufaa ya kufuata huduma hiyo Muhimbili au JKCI.

Alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya idadi ya wagonjwa  yanayohusika na moyo kuzidi kuongezeka kila kukicha ambapo wamekwisha omba ruhusa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali ya magonjwa ya moyo ya Jakaya Kikwete ili kuwasaidia katika kutimiza azma hiyo.

“Wenzatu wamekubali kutusaidia na tumeingia mkataba wa awali kuhakikisha tunafanikisha hili, ambapo kwa kuanzia tunaanza kupeleka madaktari wetu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Jakaya Kikwete kujifunza zaidi juu ya huduma hizi huku uongozi wa hospitali ukiendelea kununua vifaa hasa vipimo” alisema Twisa

Alisema kuwa wakati utaratibu huo ukiendelea watakuwa na klinik itakayofanyika kila mwezi katika hospitali hiyo ambapo madaktari kutoka hospitali hizo mbili wabia watakuwa wanakuja kutoka huduma hali itakayosaidia kuwapatia wagonjwa unafuu, lakini pia kupunguza gharama za matibabu, safari na malazi wanapofuata huduma Dar-es-salaam.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dr. Mohammed Janabi alisema kuwa Matatizo ya moyo yanaongezeka kila kukicha nchini hasa mikoa ya kanda ya kaskazini ambapo kwa uchunguzi wa awali wamebaini kuwa unasababishwa na matumizi ya chumvi nyingi hasa kutokana na ulaji wa nyama, lakini pia matumizi ya sukari hasa kwenye juisi na bia sambamba na kudharau mazoezi.

‘Vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa moyo vinaongoza kwa sasa duniani kwa asiliamia 32 ambayo ni sawa na watu milioni 18 wanakufa kila mwaka kwa ugonjwa huo huku kwa Tanzania kila watu wanne mmoja anakufa kwa ugonjwa wa moyo.., nadhani ndugu zangu mnapata picha jinsi janga hili linakuja kuwa kubwa hivyo sisi kama Muhimbili na Jakaya kikwete hatuwezi kupangua hili”

Alisema kuwa kwa sasa wako katika utekelezaji wa program maalumu ya kuweka kambi ya kliniki katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Dodoma kwa ajili ya kutoa huduma hizi hivyo kuipongeza hospitali ya Seliani kwa kufungua kitengo hiko ambacho kitakuwa msaada mkubwa wa kupunguza foleni kwao.

Zaidi Dr. Janabi aliwataka wananchi kuhakikisha wanakata bima za afya kwa ajili ya kupunguza gharama za matibabu ya ugonjwa wa moyo, ili kupunguza vifo vitokanavyo na wagonjwa huo kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu.

“Jamani kateni bima za afya kwani zina umuhimu mkubwa sana hasa kipindi hiki ambacho huduma za matibabu ya ugonjwa wa moyo zinaenda kupanda kutokana na uendashaji wake, lakini pia bima zitasaidia kupata huduma kwa haraka na kupunguza pia idadi ya vifo” alisema Dr. Janabi

Mbali na hilo aliwataka vijana kuwa na mwenendo mzuri wa maisha na kuachana na matumizi makubwa ya pombe kali, uvutaji wa sigara, shisha na Msongo wa mawazo laiki pia wafanye mazoezi ili kuepuka unene kupita kiasi

 

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!