Ngorongoro wapokea faru weupe 18 kutoka Afrika kisini

 


Arusha. 

Serikali imepokea jumla ya faru 18 kutoka nchini Afrika kusini kwa ajili ya kuanza mradi wa upandikizaji wa wanyama hao hapa nchini.


Ujio wa faru hao uliofanikishwa kwa ushirikiano na kampuni ya utalii ya Andbeyond ya Afrika kusini, unafanya rasmi Tanzania kuwa  na wanyama hao ambao wamepokelewa katika kreta iliyoko ndani ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro( NCCA)


Faru hao ambao wanaanza kupandikizwa katika kreta ya Ngorongoro ni sehemu ya faru 36 ambao wataletwa kwa awamu hapa nchini kwa ajili ya uhifadhi, utafiti na Elimu kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Akipokea Faru hao katika eneo la kreta ya Ngorongoro, Waziri wa Maliasili na utalii, Balozi Dk Pindi Chana amesema kuwa ujio wa faru hao ni matokeo ya ushirikiano wa kimataifa katika uhifadhi ambao Tanzania imejiwekea kwa ajili ya utunzaji wa wanyama pori.

"Huu ni sehemu ya ushirikiano wetu kimataifa wa utunzaji, uhifadhi na ulinzi wa wanyama pori ndio maana Tanzania tumekuwa tukiwapeleka pia wanyama nje mfano Tembo tuliowapeleka India na ndege Tausi tuliwahi kupeleka kwa jirani zetu Kenya" amesema Dk Chana.

Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika uhifadhi nchini na sasa ina idadi kubwa ya wanyama hata walio hatarini kutoweka duniani akiwemo Faru lakini pia ni kinara wa wanyama kama Simba na nyati na sasa inatengeneza historia nyingine ya kuwa na aina hiyo ya faru inayoongeza idadi ya spishi ya wanyama nchini.

"Na matunda makubwa ya uhifadhi immeyaona ikiwemo kusaidia kutimiza malengo yetu ya utalii tuliyokuwa tumejiwekea nchini ambayo hadi sasa tumeingiza watalii milioni 5.3 huku malengo  yalikuwa kutembelewa na watalii milioni Tano hadi mwishoni mwa mwaka huu".

Amesema kuwa malengo ya mapato ni Dola Bilioni sita hadi kufikia mwisho wa mwaka huu ambapo hadi sasa wameingiza Dola 3.6 Bilioni.

Dk Chana alitumia nafasi hiyo kuwataka wataalam kutoka Afrika Kusini na nchini kushirikiana kwa pamoja kuwatunza wanyama hao Ili waweze kustawi na kutimiza malengo ya kuhifadhi kizazi chao.

Kwa upande wake kiongozi wa kimila wa Jamii ya Makhasa, iNkosi Gumede Zwelinzima ambae ni mjumbe wa bodi ya Isimangaliso nchini Afrika Kusini, amesema lengo la kuwaleta faru hao hapa nchini Tanzania ni kwa ajili ya kuwahifadhi kizazi chao kutokana na kushamiri kwa matukio ya ujangili nchini kwao kunakotishia kizazi hicho kupotea baadae.

" Kama mnavyojua Afrika Kusini ndio kinara kwa faru wengi Afrika lakini matukio ya ujangili yanatutishia ndio maana tumeanza kusambazwa kizazi hiki katika nchi za Botswana, Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na leo Tanzania" amesema.

Amesema kuwa nchi ya Afrika Kusini imekumbwa na janga kubwa la ujangili wa faru tangu mwaka 2008, ambapo zaidi ya faru 10,000 wamepotea kufikia mwaka 2023.

"Licha ya changamoto hizi, tumefanikiwa kukuza idadi ya faru weupe kwa utulivu, na tumeona ni vema kufanya uhamishaji wa faru kwenda maeneo mengine lengo kutunza spishi hii"

"Na leo, tunajivunia kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa faru nchini Tanzania kwa kutoa faru weupe wa kusini kwenu baada ya Utafiti wa wizara hii kuthibitisha kuwa Ngorongoro ni makazi bora kwa ukuaji wa faru hawa" amesema mwakilishi huyo kutoka Afrika kusini..

Amesema Mradi huu unalenga kuanzisha kundi la faru wa kuzaliana, ambao hatimaye watasaidia kuimarisha idadi ya faru katika maeneo mengine yaliyohifadhiwa nchini Tanzania na wanaamini wataleta thamani ya kudumu, wakichangia uhifadhi na fursa za kiuchumi kwa vizazi vijavyo.

Awali Kamishna wa uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCCA) Dk Elirehema Doriye amesema kuwa mradi huo wa kupandikiza faru hao nchini itasaidia kwa uhifadhi, Utafiti na Elimu nchini na kuleta manufaa zaidi kwa vizazi vijavyo.

Amesema kuwa faru hao 18 ambao wamewekwa kwenye kreta ya Ngorongoro wametengenezewa uzio maalum kwa ajili ya uhifadhi lakini pia kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wao wa kuzoea taratibu mazingira ya chakula na hali ya hewa ya hapa nchini kabla ya kuwaachia rasmi kusambaa.

Nae mkurugenzi wa Utafiti  kutoka taasisi ya Utafiti wa wanyama pori nchini, 'Tawiri' Dk Julius Keyyu, amesema kuwa kabla ya kuwaleta faru hao wakianza kufanya Utafiti wa mazingira, hali ya hewa na magonjwa katika eneo hilo wakaona wanastahimili kustawi hapo.

"Wanyama hawa wanakula majani, lakini Adui yao mkubwa ni ujangili na magonjwa ya mdudu Mbung'o ambao hapa hawapo hivyo tunaamini watastawi na kukuza vema kisha wanaweza kusambazwa katika hifadhi zingine kama Mikumi na Burigi chato kwani mazingira nayo yanaruhusu" amesema.

Nae mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa NCCA, generali mstaafu venance mabeyo amesema kuwa wajumbe wote watakuwa karibu na mradi huo kutoa maelekezo ya mara kwa mara kuhakikisha wanyama hao wanatunzwa na kuhifadhiwa vema sambamba na kupimwa mara kwa mara dhidi ya maendeleo yao ya magonjwa.

Mwisho.
Post a Comment (0)
Previous Post Next Post