Bertha Mollel, Arusha
Jumla ya wananchi 1844 wamefanikiwa kuhudumiwa katika kiliniki ya msaada wa kisheria unatolewa na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia kampeni ya Samia Legal Aid.
Wananchi hao wamepata msaada huo, katika kliniki ya msaaada wa kisheria inayoendelea jijini Arusha ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani machi 8,2025 .
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkurugenzi wa huduma za msaada wa kisheria, Esther Msambazi kutoka wizara ya katiba na sheria amesema kuwa wameweza kuwafikia wananchi 1844 huku wengi wao wakiwa ni wanaume .
Amesema kuwa migogoro iliyoongoza kuwasilishwa katika kliniki hiyo ni migogoro ya ardhi ikifuatiwa na migogoro ya madai.
“Hii imekuwa tofauti na mikoa mingine ambayo mingi baada ya migogoro ya ardhi inafuatiwa na masuala ya ukatili wa kijinsia na mirathi” amesema.
Amesema kuwa kwa siku saba walizohudumu Mkoani Arusha wamefanikiwa kuwafikia wananchi 1844 na kupokea migogoro 677 na kati yake migogoro 136 imetatuliwa.
“Tunapozungumzia utatuzi ni kwamba tumefanikiwa kuwapatanisha wahusika wa pande mbili na kutatua changangamoto zilizokuwa zikiwakabili na wameondoka wakiwa na amani" amesema Msambazi.
Amesema kuwa katika kliniki hiyo wanaume wameongoza kuleta mashauri yao.
"Migogoro mingi imewasilishwa na wanaume, inawezekana wanaume wana changamoto zaidi kuliko wanawake lakini pia inawezekana wamezibeba changamoto hizo kama baba wa familia ndio maana tumeona wengi wamejitokeza kuziwasilisha,"Ameeleza
Ameendelea kusema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha wanawa elimisha wananchi katika ngazi za kijamii kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisheria na namna gani wanaweza kuifikia haki na kutatua migogoro ambapo hadi kufikia february 25,2005 wameshatekeleza kampeni hiyo mikoa 22.
Mmoja wa wananchi waliohudumiwa katika kliniki hiyo Miongoni mwa wananchi waliohudumiwa katika kliniki hiyo Theresia Mitawas Mollel mkazi wa Sokon One, amesema kuwa amepata msaada wa kisheria ambao anaamini utamsaidia katika utatuzi wa mgogoro wa mali za baba yake anazopambania kwa miaka miwili sasa.
“Mimi nimekuja hapa kuomba msaada baada baba yangu kufariki mwaka jana na wasimamizi wa mirathi kuteuliwa ambao ni kaka zangu, wamegoma kugawa mirathi huku wakiendelea kulima na kuuza mashamba ya familia”;
“Nimehangaika mahakamani naambiwa nije na hati ya kifo na nyaraka zingine ambazo ndugu zangu ndio wanazo na wamekataa nazo na baadae kwenda kwa Mkuu wa wilaya nazungushwa na ofisi ya mwanasheria kila kukicha, hivyo leo nimeshukuru nimepata msaada” amesema.
Theresia ameiomba serikali kuongeza siku za kliniki hiyo ili aweze kupata haki yake lakini pia isaidie na watu wengi zaidi ambao bado wanateseka na migogoro ya ardhi.
Mwisho