Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda ameingia katika vita vikali vya maneno na M'bunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo.
Vita hiyo awamu hii inahusisha taarifa za jaribio la wizi wa fedha kiasi cha sh252 milioni za Jiji la Arusha zilizofichuliwa na Gambo.
Wizi huo unadaiwa kutaka kutekelezwa na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya jiji la Arusha, baada ya kudai kiasi cha Sh552milioni kwa ajili ya ununuzi wa eneo la eka sita badala ya thamani halisi ambayo ni sh300milioni.
Kwenye ziara yake katika kata ya Muriet mashariki lilipo eneo hilo, Gambo alifichua taarifa hizo kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi na kusema kuwa wataalam wa manunuzi walileta mahitaji wa Sh552 kuwa gharama ya eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa shule lakini baada ya kufuatilia wakagundua muuzaji anahitaji milioni 300 pekee hivyo kuwa na nyongeza ya sh252milioni zilizobambikwa.
Baada ya kupata taarifa hizo, Makonda jana wakati akifungua kikao maalumu cha baraza la madiwani kwa ajili ya kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti ya jiji la Arusha kwa mwaka wa fedha 2025/2026 alitoa amri kwa Ofisi ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya kufuatilia taarifa hizo kama ni za kweli wahusika wote wachukuliwe hatua za kisheria.
“Jana nimekaa nasoma mahala naona taarifa za ununuzi wa eneo la shule halafu kuna sh252milioni zinataka kupigwa, nikajiuliza hii kivipi tena, Sasa mtahiki meya baadae nataka kupata taarifa ya jiji, hizo milioni 252 zinazosemwa zimepigwa, ziko wapi na waliojaribu kuiba hizo hela nataka niwakute kituo cha polisi”.
“Maana haiwezekani watu watuchukulie tu mzaha mzaha, wananchi hawa wanalipa kodi jamani, hivi wewe fikiria kuna barabara haijajengwa halafu kuna milioni 252 zimepigwa mahala, hivi nyie mtapewa kura tena kweli, watawaamini kweli, sasa kwanini mnafanya hivyo?”Ameuliza Makonda na kuendelea;
“Naomba Takukuru (Taasisi ya kuzuia na kupambania na Rushwa) waanze kufanya yake na mtandao wote wa usalama na kama kuna mtumishi wa umma amehusika na taarifa zake zipo wasimamishwe kazi na uchunguzi uanze” amesema Makonda.
Makonda pia amewaonya wajumbe hao kuacha kuzungumza mambo ya ndani ya jiji kwenye mikutano ya hadhara na badala yake wawasilishe kwenye vikao ili viweze kufanyiwa kazi haraka na kutatuliwa.
“Lakini pia najiuliza kwanini mtu unaenda kuongelea kwenye mikutano ya hadhara kwanini msikae kwenye vikao mkasema? Sasa mkiwaambia wananchi hivyo si wanawaona nyie wote wezi? ndio maana nasema jamani kaeni kwenye vikao ili taarifa kama hizi mnasulubiana huku huku wenyewe na mambo mazuri yanaenda kwa wananchi”;
"Halafu msikae kuwindana kuangaliana mapungufu tu, maana mojawapo ya dalili ya umaskini ni majungu kama haya, fitina na ushirika, acheni haya mambo, kama kuna taarifa mtu unayo mambo hayaendi vizuri tupe, kwani hatutakiwi kucheza na hisia za wananchi, kama kuna ushahidi leta tuchukue hatua sio tuchukulie majukwaa ya kisiasa kusema kuna wizi kuna wizi halafu tume iundwe ionekane hakuna wizi".
Katika salamu zake za kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufungua kikao hicho, diwani wa Kimandolu Abraham Mollel amesema kuwa anaefanya hayo yote ni M'bunge Gambo na amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara.
"Kiukweli ametuchosha sana, ukiangalia hata vikao hahudhurii kazi kwenda kusema mambo hovyo huko nje, sasa tunakuomba Mkuu wetu kwa upendo wa dhati tulionao na wewe tunaomba mda ukifika chukua fomu ya kugombea ubunge wa Arusha mjini na sisi madiwani tuko nyuma yako kukuunga mkono " alisema Mollel huku alipigiwa makofi na baadhi ya madiwani.
Hata hivyo baada ya hilo, Makonda hakujibu chochote zaidi ya kuomba ruhusa ya kuondoka katika kikao hicho kwa ajili ya kuendelea na majukumu mengine.
Gambo ajibu mapigo.
Akizungumza leo Februari 25,2025 jijini Arusha na vyombo vya habari, Gambo amesema kuwa kauli ya madiwani hao imetengenezwa na Makonda mwenyewe.
Amesema kuwa baada ya kuibua taarifa hizo alitegemea wahusika kuumia kuzibiwa fedha hizo hivyo hashangai kauli zao za kumponda.
"Lakini zaidi nitegemea kuona hatua zinachukuliwa dhidi ya watu waliokuwa na nia ovu ya kuiibia serikali kwa kubambika fedha ya ziada ambayo bila kusimama kidete maana yake zingeibiwa".
Hata hivyo amesema kuwa ameshangaa madiwani hao badala ya kutoa ushirikiano wahusika wakamatwe wanaibuka na hoja ya nafasi ya ubunge.
"Sasa nitoe rai kwa chama changu na serikali kuwa, Mimi kama M'bunge niliyeko madarakani nawajibika kutekeleza majukumu yangu na wajibu wangu wa kutetea maslahi ya wananchi na matumizi mabaya ya fedha za wananchi";
"Hivyo kama kuna mtu yoyote au kiongozi yoyote anaetamani nafasi ya ubunge hakuna anaemkataza asubiri mda ufike na taratibu zitangazwe halafu aje uwanjani aone kama Ngoma ya watoto inakesha sio kutumia madiwani kuwatengeneza wamuombe agombee ubunge" amesema Gambo.
Akizungumzia hoja ya kukimbia katika kikao hicho kabla ya kuisha, Gambo amesema kuwa alihudhuria kikao kwa ajili ya kujadili maswala ya bajeti pekee kama ajenda kuu na baada ya kumalizika aliondoka kuwahi majukumu mengine.