![]() |
Suzan Mary Shawe (75) |
Arusha.
Chama cha mawakili Tanganyika (TLS) kimeingia katika mgogoro mzito huku chanzo ikiwa ni kuvamiwa, kushambuliwa na kujeruhiwa kwa Raia wa kigeni Suzan Mary Shawe (75)
Mzungu huyo, (Suzan) raia wa afrika kusini, alivamiwa na kushambuliwa kisha kujeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake na kundi la vijana wenye silaha za jadi January 21,2025 saa 3:00 asubuhi huko nyumbani kwake eneo la Njiro jijini Arusha.
Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kupitia kwa kamanda wake SACP Justine Masejo alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa wamemkamata wakili wa kujitegemea Valerian Qamara pamoja na dereva bodaboda Benjamin Paul (19) kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
![]() |
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha Justin Masejo |
Kamanda Masejo alisema, Suzan alishambuliwa na watu waliotumwa na wakili Qamara kwa nia ya kumtoa kwa nguvu kwenye makazi yake kwa madai ya kutolipa kodi ya nyumba.
Hata hivyo hatua hiyo Wakili Qamara aliyekuwa mtetezi wa mmiliki wa nyumba anayoishi mzungu huyo (Suzan) alishangazwa kuhusishwa na tukio hilo huku akidai majibizano yao yalikuwa ni ya barua kwa barua.
Pia amedai siku ya tukio wala hakuwepo Arusha hivyo hahusiki kwa lolote juu ya shambulio la Suzan.
Mgogoro waibuka
Hata hivyo Jeshi la Polisi liliendelea kumshikilia Wakili Qamara bila dhamana kwa siku tatu mfululizo.
Hata hivyo wakili Qamara baadae ilipatikana tetesi za kubadilishiwa makosa kutoka shambulio la awali hadi wizi wa kutumia silaha (Amri robbery)hali iliyoibua hisia kwa mawakili na viongozi wa TLS.
Awali akizungumza na waandishi wa habari jumapili January 26,2025, mwenyekiti wa TLS Kanda ya kaskazini George Njooka amesema kuwa dhamana ni haki ya mtuhumiwa yoyote Ile ambae anatuhumiwa kwa makosa yenye dhamana.
"Lakini baada ya kuona hawataki kumpa dhamana wakabadilisha mashtaka yake kutoka shambulio hadi wizi wa kutumia silaha ambayo imewapa jeuri ya kunyima hata ndugu na familia wengine kumsalimia mwenzetu akiwa mahabusu" amesema Wakili Njooka.
Kitanzi cha TLS na Jeshi la polisi
Kutokana na hilo, wakili Njooka amesema wameazimia kuwashitaki maofisa wanne wa Jeshi la Polisi akiongozwa na kamanda wa Polisi Mkoa, kamanda wa Polisi Wilaya (ODC),Mpelelezi wa Wilaya na Mkuu wa kituo cha Polisi cha kati lakini pia Suzan (mzungu aliyeshambuliwa).
"Pia tumekubaliana kupeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ambayo yatatoa kinga na muongozo wa hii kamata kamata ya mawakili wanapotekeleza majukumu yao au kwa makosa ya wateja wao ili kututisha"
"Hii itatisaidia kuondokana na misuguano ya mara kwa mara na jeshi la polisi na kuchukuliana kama maadui wakati wote tuko katika harakati za kutafuta ugali wetu "amesema.
Mbali na hilo wameazimia kuwaburuza maofisa hao kwenye kamati za maadili Ili waweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
"Na kubwa kuliko tunamewawekea mgomo wa kuwawakilisha kwenye kesi hiyo tunayowafungulia na mmoja wetu akifikia kutusaliti tutamtenga" amesema Njooka.
Awali akisimulia tukio hilo,
Akizungumza na waandishi wa habari, Suzan alisema January 21, Mwaka huu, majira ya saa tatu asubuhi akiwa nyumbani kwake, vijana zaidi ya 20 wakiwa na mapanga, Nyundo na Nondo walimvamia nyumbani na kuanza kumshambulia kwa silaha hizo na kumjeruhi kwa kumpiga nyundo kichwani na kumvunja mkono wa kulia kwa kumpiga na nondo huku wakiwafungia ndani mbwa wake wa ulinzi.
Amesema katika tukio hilo, watu hao pia walimpora simu zake tatu za Mkononi pamoja na za wafanyakazi wake na walivamia chumbani kwake na kuiba fedha kiasi cha Shilingi milioni saba pamoja na Dola 2000 za kimarekani.
"Nilikuwa chumbani kwangu nikasikia kelele, wakati naamka nione kwa dirishani nini kinaendelea ndio dada wa kazi alikuja chumbani kwangu na kuniambia kunatatizo kubwa nje" amesema Suzan na kuongeza ;
"Nilifunga mlango wangu kwa komeo kujihami lakini baada ya muda walikuja na kuvunja mlango wangu wakaingia chumbani kwangu na kunikamata na kuanza kunipiga na nyundo kichwani kisha kuniburuza kutoka gorofani hadi chini kisha nje ya geti nikiwa mtupu bila nguo".
"Wakati hayo yote yakiendelea walikuwa wananiambia nitoke ndani ya nyumba kwa sababu nadaiwa kodi wakati nimeishi hapa kwa zaidi ya miaka 20 na Marehemu mume wangu aliyefariki miaka miwili iliyopita tukilipa Kodi ya mwaka mzima na mwisho nililipa Desemba mwaka jana" .
Amesema kuwa wakati wengine wakitekeleza kipigo hicho wengine waliendelea kupekua chumba chake na kumwaga vitu ambapo waliondoka na simu pamoja na fedha za akiba alizokuwa nazo.
Mmoja wa mfanyakazi wa raia huyo, Ayubu Malolo alisema majira ya saa tatu walifika watu wakiwa na pikipiki sita wakiwa na mapanga na Nyundo na kuanza kuwahoji kwanini wanaishi kwenye nyumba hiyo bila kulipa kodi.
"Sikuwa na jibu nao, ndio wakaelekea kwenye chumba cha bosi wangu, na kuanza kuvunja mlango na kuingia chumbani " amesema.
"Akaanza kusema 'mtoeni huyo mzungu' walianza kumburuza akiwa uchi hadi getini huku wakimpiga na nyundo kichwani, walipofika getini walikuta watu wamejaa ndipo walipomuacha na kukimbia kwa pikipiki zao"amesema Malolo.
Mwisho ......