Asema hakuna mtu yoyote anayeweza kuzuia kusema matatizo na kero za wananchi kwani huu sio wakati wa kulindana.
"Barabara iko hadharani ni lazima tusemee kero zake hadharani sio chumbani, bila kujali nani anafurahi au nani anachukia" amesema
Arusha
Wakati Mkutano wa 18 wa Bunge la Tanzania ilitarajia kuanza vikao vyake leo mjini Dodoma, M'bunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo ametaja baadhi ya kero anazotarajia kuziwasilisha katika vikao hivyo.
Gambo amesema mbali na kwenda kusemea changamoto zinazozikabili vituo vya afya na zahanati lakini pia ataongelea umuhimu wa wananchi wa kata ya Olmoti kupewa kipaumbele cha ajira kwenye mradi wa ujenzi wa uwanja mkubwa wa Afcon unaoendelea jijini Arusha.
Pia amesema kuwa barabara imekuwa kero kubwa katika Jiji la Arusha huku baadhi yake zikisuasua ujenzi wake licha ya fedha kutolewa kwa ajili ya kusaidia kutatua kero hizo.
Katika ziara yake hivi karibuni ya kutembelea barabara ya Engosheraton, Gambo alishangazwa na kudorora kwa mradi huo huku wananchi wakilia kuharibiwa miundombinu ya maji safi, taka na mitaro yao.
Mwanaisha Juma ameiomba serikali iongeze nguvu katika usimamizi wa kazi hiyo kuhakikisha ujenzi unaisha kwa wakati Ili kupunguza mateso wanayoyapata kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 4.8 iliyoanza kujengwa November 2023 ikitarajia kukamilika February 2025 kwa gharama ya Sh4.6 Bilioni hadi sasa imekamilika kwa asilimia 60 pekee.
Gambo alitumia nafasi hiyo, kuwataka TARURA kuongeza jitihada za kusimamia mkandarasi atimize wajibu wake wa kumaliza kazi hiyo kwa wakati kunusuru wananchi wanaoteseka kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
"Wakati mwingine tunapowaambia hivi mnasena M'bunge mkorofi, Mimi siwezi kuwa mpole kama mambo hayaendi vizuri kwani natumia nguvu kubwa kuhakikisha nazisemea miradi hii Bungeni na kweli inaonekana ina uhitaji na fedha zinapitishwa zinakuja"
"Leo fedha zije na mambo hayaendi sawa eti ninyamaze niache kusemea kero za wananchi wangu wakati wanateseka kisa Kuna mtu hataki zisemwe".
"Mambo yakienda vizuri siwezi kuwa mkorofi lakini mambo yakiendelea hivi hata bungeni nitasema wakandarasi wababaishaji walioko kwenye majimbo yetu wasipewe kazi" amesema Gambo.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wasiogope kuwa nae kwani ataendelea kusema kero hizo hadharani kwani ndipo kutakapopatiwa ufumbuzi.
"Niwaambie wazi kuwa hakuna mtu yoyote ambae anaweza kutuzuia kusema matatizo na kero za wananchi wetu kama hawataki tuseme wafanye kazi kama kuna mradi utekelezwe kwa wakati sio kulindanalindana hiyo biashara nimekataa" amesema Gambo na kuongeza;
"Bahati nzuri Rais wetu mama Samia amesikia kilio cha wananchi hawa akaleta fedha halafu mtu mmoja anakuja kuleta ujanja ujanja eti tusiseme haya mambo hadharani anataka tusemee chumbani, leo nasema barabara iko hadharani ni lazima tusemee hadharani bila kujali nani anafurahi au nani anachukia" amesema Gambo.
Mwisho...