Tizama wananfunzi wa Shule ya Arusha Science Sekondari walivyotengeneza gari la umeme

 


Arusha . Wanafunzi wanaosoma kidato cha tano katika shule ya Sekondari Arusha Science iliyopo mkoani Arusha wametengeneza gari linalotumia mfumo wa umeme ikiwa ni utekelezaji wa mafunzo kwa vitendo katika nyanja ya ubunifu na matumizi ya Sayansi na teknolojia.


Gari hilo linalotumia nishati ya umeme, linachajiwa kwa masaa sita na kuweza kutembea hadi kilometa 70 likiwa na mzigo na baada ya hapo linahitaji kuchajiwa tena.


 

Innocent Mtei (18) na Diana Mwacha (17) ni miongoni mwa wanafunzi waliotengeneza gari hilo ambapo wamesema kuwa gari hilo ni ubunifu wa miaka miwili waliotekeleza wanafunzi watano wa kidato cha tano ili kukabiliana na hewa chafu angani lakini pia uhaba wa mafuta ya diseli na petrol ambayo magari mengi hutumia kama  nishati pekee.

Mwacha amesema kuwa hadi kukamilika kwake tayari gari hilo limegharimu zaidi ya Shilingi milioni sita katika utengenezaji.

“Gari hili tumefanikiwa kukamilika baada ya miezi 19, na kwa sasa tunaendelea kulifanyia majaribio ya mwisho kabla ya kuanza kuliombea kibali cha kuanza kuzizalisha tutapopata ufadhili baadae” amesema Mwacha.


 

Nae Mtei amesema kuwa kwa sasa wanaweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi kwa watu wenye magari ambao wanahitaji kubadili mifumo ya vyombo vya vya usafiri kutoka kutumia mafuta hadi umeme kwa kubadili mfumo wa mzima wa Injini yake.

“Mfano hili la kwetu linaweza kuchajiwa kwa chaja yake maalumu kwa masaa sita tu kwenye soketi yoyote ya umeme wa Tanesco na kuingia kwenye kifaa chake cha udhibiti umeme kilichoko ndani ya gari na kujijaza tiyari kwa matumizi” amesema.

Amesema likiwa limejaa chaji, gari hilo linaweza kutembea spidi ya kilomita 70 kwa saa ambalo linasaidia kuokoa gharama ya ununuzi wa mafuta mara kwa mara.

“Pia ni miongoni mwa magari ambayo yanatunza mazingira kwani haizalishi hewa chafu na haihitaji kufanyiwa service mara kwa mara kama magari yanayotumia mafuta” Amesema.

Amesema wameweza kutengeneza gari hilo ili kuonyesha kwa vitendo vile vyote wanavyofundishwa  shuleni ikiwa ni muendelezo wa bunifu mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi.



Mwalimu wa Darasa hilo la kidato cha Tano katika shule ya Arusha Science, Godlisten Lema amesema kuwa ubunifu huo ni muendelezo wa bunifu nyingi zinazofanywa na wanafunzi shuleni hapo.

“Hapa tunafanya kazi kubwa ya kuibua vipaji na kuwawezesha wanafunzi kutumia sayansi na teknolojia katika kubuni mambo mbalimbali yenye kuleta suluhu kwa jamii ili kuendana na karne ya 21 ya mapinduzi ya viwanda” amesema.

Amesema kuwa utengenezaji wa gari hilo ni muendelezo wa bunifu za wanafunzi shuleni hapo ikiwemo waliowahi kutengeneza gari la kutumia nishati ya umeme wa jua (Sola) kwa ajili ya kurahisisha ubebaji wa mizigo katika maeneo mbalimbali ya viwandani.

Amesema pia wanafunzi ambao wanatengeneza roboti kwa matumizi tofauti ikiwemo ya kufanya kazi na utambuzi wa alama mbalimbali hasa za hatari ambao wanalenga kutumika katika ulinzi.

“Yote haya ni kuhakikisha wanafunzi wanapohitimu wanaweza kufanya bunifu mbalimbali kuendana na mabadiliko ya sayansi ya Teknolojia na kushindana na mahitaji ya soko la dunia katika kujipatia kipato na kuimarisha uchumi wa nchi na ukanda mzima wa Afrika” amesema.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!