Arusha.
Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC) imeingia kwenye mgogoro mkubwa na wapangaji wake zaidi ya 450 baada ya kuwapatia notisi ya kutakiwa kuhama katika nyumba zao ndani ya siku 60 hadi 90.
Wapangaji hao walioishi ndani ya nyumba hizo zilizoko Kijenge jijini Arusha kwa zaidi ya miaka 40 wamedai kuwa hawahami kwenye nyumba hizo kwani notisi hiyo haijawatendea haki kutokana na wamepewa mda mdogo sana kuhama bila kushirikishwa kwa ajili ya majadiliano ya pande zote mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mpangaji Deepak Teja amesema kuwa amepewa notisi ya kuhama ndani ya siku 60 kitendo ambacho bado ni kigumu kwake kutokana na kuwa ni mwisho wa mwaka na pia hawajashirikishwa mapema kwa ajili ya majadiiano na makubaliano.
“Sisi tumekaa hapa zaidi ya miaka 35 na wengine 40 tukichangia mapato kupitia kodi zetu na hatujawahi kusumbua inakuwaje leo watuondoe kama wakimbizi eti kuna mradi wanataka kutekeleza? Kwanini wasitushirikishe tukubaliane kwa amani? Sasa hapa hatuhami hadi waje kutueleza kisa cha taarifa hizi za ghafla” amesema.
Nae Subira Mawenya amesema kuwa taarifa hizo zimekuwa ghafla sana hivyo hawawezi kuhama na wanaiomba AICC kuwapatia angalau miezi sita ya kujipanga kutokana na mda waliopewa ni miezi ya sikukuu za mwisho wa mwaka na wanaishi na familia zao hapo hivyo ni vigumu kupata nyumba kwa haraka.
“Mimi nina familia kubwa tu hapa, ukinipa siku 60 au 90 nihame maana yake january niondoke, embu niambie nihamie wapi, tunaomba watupe angalau miezi sita tuanze kufanya mchakato wa kupata mahala pengine pa kuhamia” amesema.
Katika barua iliyoonwa na Mwandishi wa habari hizi, imetoa taarifa ya kusitishwa kwa mkataba wa kukodisha nyumba hizo zilizoko kijenge kwa madai ya kupisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika eneo hilo.
“Kwa mujibu wa Kipengele 4 (vii) cha Mkataba wa Kukodisha kinachosema, "Endapo Mwenye Nyumba atahitaji kurejesha nyumba kwa ajili ya matumizi yake mwenyewe, notisi ya siku tisini (90) itatolewa kwa Mpangaji kwa anwani iliyoonyeshwa hapo juu au kwenye mali husika, na baada ya kumalizika kwa muda wa notisi hiyo, Mpangaji atatakiwa kuikabidhi mali hiyo kwa Mwenye Nyumba" ilisema sehemu ya barua hiyo na kuongeza;
“AICC inakupa notisi ya siku tisini (90) ya kusitisha Mkataba wako wa Kukodisha kuanzia tarehe ya kupokea barua hii ili kupisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika eneo hili. Tafadhali hakikisha kuwa umehamisha mali zako zote na kuwa umetoa nafasi hiyo ifikapo tarehe husika”
Akithibitisha kutoa notisi hizo, Afisa uhusiano na mahusiano wa AICC Assah Mwambene amesema kuwa wametoa barua hizo kwa wapangaji wake kwa ajili ya kupisha eneo hilo kufanyika uwekezaji mwingine.
“Hakuna taratibu wala sheria tumekiuka kwenye mpango huu, kikubwa wanatakiwa kuhama kupisha hilo eneo kwa ajili ya kufanyika uwekezaji, hao wanaosema hawahami hatuwezi kuwasemea chochote kwa sasa bali tusubiri mda waliopewa ukifika taasisi itasema” amesema Mwambene.
Mwisho…..