China kuipiga jeki Tanzania katika sekta ya utalii wa miamba, waanza na ujenzi wa kituo cha Taarifa Ngorongoro-Lengai geopark

 NGORONGORO-LENGAI KUNUFAISHA WATALII ...

 

Arusha

 Serikali ya China imeahidi kuisaidia Tanzania kufikia lengo lake la kuvutia watalii milioni 5 ifikapo 2025, sambamba na kuzalisha mapato ya dola bilioni 6 kutoka sekta ya utalii.

Kulingana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)hadi mwezi Julai 2024, idadi ya watalii waliowasili Tanzania ilikuwa 2,026,378, na hivyo kuwepo na pengo la watalii 2,973,622 ili kufikia lengo hilo mwaka 2025.

Pia lengo la serikali ni kuzalisha dola bilioni 6 kutoka kwa watalii ifikapo mwaka 2025 lakini hadi julai, 2024, mapato kutoka sekta ya utalii yalifikia dola bilioni 3.534, hivyo kuacha pengo la dola bilioni 2.466.

 Ngorongoro-Lengai Wilayani Karatu ...

Akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi wa mradi wa Kituo cha Taarifa cha Ngorongoro-Lengai Geopark, kilichofadhiliwa na serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingian, alisema wako tayari kuisaidia Tanzania kufikia malengo yake ya utalii.

"China, kama rafiki wa muda mrefu wa Tanzania, imeendelea kuunga mkono maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania kwa zaidi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia. Katika miaka ya hivi karibuni, tumekuwa tukisaidia kwa vitendo kukuza sekta ya utalii, na tunaahidi kuendelea kutoa msaada ili kufikia malengo yake," alisema.

 NGORONGORO-LENGAI KUNUFAISHA WATALII ...

Alisema kwamba, katika kudumisha ushirikiano huu, China imefanya mengi kwa vitendo, na mradi wa Kituo cha Taarifa cha Ngorongoro-Lengai Geopark ni mradi wa kwanza wa msaada wa uhifadhi wa urithi wa kijiolojia wa China nje ya nchi.

"Huu ni upendeleo mkubwa kwa Tanzania kwa sababu China haijawahi kufanya hili kwa nchi nyingine yoyote duniani. Mradi huu ni muhimu katika utekelezaji wa Mpango wa Ukanda na Barabara (Belt and Road Initiative) na vilevile Mpango wa Maendeleo ya Kijani kati ya China na Afrika," aliongeza.

"Zaidi ya hayo, mradi huu utakuwa kiungo muhimu katika ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi zetu mbili, na kutoa jukwaa jipya la kubadilishana na kushirikiana katika nyanja za utalii na utamaduni."

"Tanzania imebarikiwa na rasilimali nyingi za asili za utalii, ikiwa ni pamoja na maeneo ya Urithi wa Dunia kama Mlima Kilimanjaro,  Hifadhi ya Serengeti, ambayo ni makazi ya wanyamapori wengi zaidi barani Afrika, Zanzibar, 'lulu ya Bahari ya Hindi,' na Hifadhi ya Ngorongoro, ambapo tupo leo, Hivyo, kufikia malengo haya ya utalii inawezekana kabisa," alisema.

Aliongeza kusema kwamba China imefanya juhudi kubwa kutangaza utalii wa Tanzania, akimtolea mfano muigizaji maarufu wa China, Kim Dong, ambaye pia ni Balozi wa Utangazaji wa Utamaduni na Utalii wa uhusiano kati ya China na Tanzania, na ambaye alishiriki katika filamu ya Tanzania Amazing.

"Filamu hii imeenezwa sana nchini China na imepokea mwitikio mkubwa. Zaidi ya hayo, kampuni nyingi za Kichina zimechangia kuboresha miundombinu ya utalii ya Tanzania kwa kushiriki katika miradi ya viwanja vya ndege, barabara, na hoteli. Sasa, kituo hiki cha taarifa kitawaleta watalii wengi zaidi hapa Tanzania," alisema.

Katika taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni na Jiolojia, Dk. Agness Gidna, alisema kwamba kituo hicho cha taarifa, kitakachogharimu zaidi ya bilioni 22 hadi kukamilika, kitakuwa ni mfano wa maonyesho ya vipengele mbalimbali vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

 NGORONGORO-LENGAI KUNUFAISHA WATALII ...

"Kituo hiki kitakuwa kama makumbusho ya kutoa taarifa kuhusu urithi wa kijiolojia wa Hifadhi ya Ngorongoro, ikiwa ni pamoja na historia ya milima na mabonde, wanyama waliopo, mioto ya asili, mto na maji, na umuhimu wake kwa jamii zinazozunguka Ngorongoro," alisema.

"Vituvutio vingine vitakavyokuwepo katika makumbusho hii ni Urithi wa Malikale wa Ngorongoro, Utamaduni wa jamii za Wawindaji, na ukumbi wa maonesho wenye uwezo wa kubeba zaidi ya watu 100 ili kuona Ngorongoro kwa njia ya moja kwa moja."

Dk. Gidna aliongeza kuwa, hii itasaidia watalii wanaotembelea Ngorongoro kuelewa wapi wanataka kwenda na nini kinawavutia zaidi, na pia kutoa hadithi ambazo wataweza kusimulia wanapoondoka Tanzania kurudi makwao.

 NGORONGORO-LENGAI KUNUFAISHA WATALII ...

Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, alisema kuwa ujenzi wa Kituo hiki cha Taarifa utasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini na aliwataka viongozi wanaosimamia mradi huu kuhakikisha wanawahusisha wananchi.

"Natoa wito kwenu, viongozi, hakikisheni wananchi wanashirikishwa kwa kila jambo, hii itasaidia katika masuala ya usalama, utunzaji na hata kufikia malengo yaliyowekwa," alisema Chana.

Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dkt. Elirehema Doriye, alisema mradi huu utawasaidia watalii kutoka mataifa mbalimbali kufurahia utalii wa miamba, na wakazi wa wilaya za Karatu, Ngorongoro, Monduli na Longido watakuwa sehemu ya wanufaika wa mradi huu.

Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu), alisema kuwa Bodi ya NCAA na Menejimenti wanashirikiana na Mkandarasi wa makumbusho kuhakikisha kazi inaendelea kwa viwango vya kimataifa, kuzingatia ubora, na kuhakikisha jengo hili linakamilika ifikapo Mei 2025 ili watalii waanze kupata huduma kupitia vivutio vitakavyokuwepo katika makumbusho hiyo.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!