Jumla ya timu nane zimekutana jijini Arusha kushiriki bonanza maalumu la wafanyakazi wa wakala wa misitu Tanzania(TFS) kwa ajili ya kuboresha mahusiano na mashirikiano baina yao.
Bonanza hilo linalofanyika kwa siku nne jijini Arusha pia lina melengo ya kuimarisha ulinzi wa rasilimali misitu lakini pia kuimarisha mahusiano na jamii dhidi ya uhifadhi wa miti nchini.
Mratibu wa bonanza hilo, Afisa Muhifadhi Mwandamizi kutoka TFS Marcel Bitulo amesema bonanza hilo litashirikisha timu nane kutoka kanda zote za huduma za misitu katika michezo ya soka, mpira wa mikono na riadha.
Akitaja kanda hizo amesema ni pamoja kanda ya kati, kanda ya kaskazini, kanda ya ziwa sambamba na kanda ya magharibi pamoja na shamba la miti SAOHIL, nyanda za juu kusini, na kanda ya mashariki.
“Mbali na malengo ya kujenga mahusiano na ushirikiano lakini pia mashindano haya ni muhimu kwa afya zetu katika kulitumikia taifa na zaidi tutayatumia kuangalia wachezaji wazuri watakaoweza kutuwakilisha katika michuano ya Shimuta msimu ujao itakayofanyika Mkoani Tanga” amesema Bitulo.
Akizindua bonanza hilo, Kamshina Msaidizi Mwandamizi wa
TFS CPA (T) Peter Mwakosya akimwakilisha kamishna wa Uhifadhi wa misitu nchini
aliwataka viongozi wa kanda zote kuhakikisha wanatenga bajeti za michezo kwa
ajili ya kusaidia mashindano hayo kuwa ya kila mwaka.
"kufanya hivyo kutawezesha shughuli za michezo kwa askari wetu wa uhifadhi ikiwa ni njia pekee ya kuendelea kuimarisha afya zao, na ukakamavu zaidi" Amesema.
Mchezaji Ramia Konyo wa mpira wa mikono alisema mashindano kama hayo yanajenga Afya zao mahala pa kazi na mahusiano mazuri baina ya wafanyakazi ikiwemo kufahamiana na kubalishana uzoefu wa changamoto wanazokutana nazo kazini kutoka vitengo mbalimbali.
Nae Meneja Uhusiano kutoka TFS Johari Kachwamba amesema bonana hilo wanatarajia litajenga utamaduni wa wafanyakazi kufanya mazoezi kwa hatma ya afya zao hasa katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.
Mwisho…