Arusha.
Rais Dk Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, serikali inatambua changamoto za walimu na umuhimu wa kuzitatua kwa wakati ili kuwapa hamasa ya utendaji kazi wao kwa hatma ya Taifa la kesho.
Kwa kutambua hilo, Rais Dk Samia amesema kuwa kila uchumi unavyoruhusu, ndio na serikali itakavyojitahidi kuwakumbuka walimu nchini katika utatuzi wa changamoto zao.
"Nimepiga simu kuwapongeza Walimu kwa sababu mnafanya kazi kubwa sana hapa nchini, na niwaambie nafahamu changamoto zenu, hivyo niwaahidi kila uchumi unavyoruhusu, tutajitahidi kuwakumbuka, namaanisha kila uchumi utavyoruhusu basi nanyi mtanufaika" amesema Rais Dk. Samia.
Dk. Samia ameyasema hayo jana kwa njia ya simu ya M'bunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo, kwenye maadhimisho ya siku ya Walim duniani iliyokwenda sambamba na ugawaji majiko ya gesi 5000 kwa watendaji hao yenye thamani ya Sh417.5 milioni.
Katika maadhimisho hayo, Rais Dk. Samia amewapongeza walimu hao kwa kukutana kwa wingi wao na kuwa na ajenda ya nishati safi ya kupikia hivyo nae kuahidi majiko zaidi kwa walimu kama mchango wake wa kuwaunga mkono.
Akizungumza katika maadhimisho hayo ya walimu wa shule za msingi na Sekondari Mkoa wa Arusha, Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga amesem sekta ya Elimu inahamasisha matumizi ya nishati safi kwa sababu ya kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na kuwaepusha na madhara ya nishati chafu kwa walimu ambao ni tegemeo kwa hatma ya Elimu ya Taifa la kesho nchini.
“Katika siku hii ya leo ya kuadhimisha siku ya walimu kauli mbiu yetu inahusu masuala ya nishati safi ya kupikia na kama mnavyofahamu Mei mwaka huu Rais alizindua Kampeni hii ya utumiaji wa nishati safi ya kupikia ikiwa na malengo ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wamefikiwa na matumizi ya nishati safi ya kupikia na sisi tumeanza na ninyi Arusha" amesema na kuongeza;
“Hivyo tunamshukuru Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo pamoja na Oryx kwa kutoa mitungi ya gesi kwa walimu 5000 ili watumie nishati safi ya kupikia na Wizara yetu tumelibeba jambo hili na tumeanza na taasisi zote za elimu ambazo zinahudumia watu zaidi ya 100" amesema Waziri huyo.
Amesema Walimu wa Arusha ambao wamepatiwa majiko ya gesi wanaandaliwa utaratibu wa kupatiwa elimu ya matumizi sahihi ya nishati hiyo ili waweze kuishusha kwa wananchi na hatimae nao watumie nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amesema kuwa amemua kutoa Zawadi ya majiko hayo kwa walimu kwa kutambua mchango wao katika kusherehekea siku hii hivyo kuwataka kila mwalimu kuwa mabalozi wa nishati safi.
“Kazi ya Rais ni kuonesha njia na sisi wasaidizi wake ni kumuunga mkono na leo tunakabidhi majiko ya gesi kwa walimu na hii ni kumuonesha mwalimu tunampenda na tunamtambua na sasa wakawe mabalozi wa nishati safi ya kupikia"
Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru kampuni ya majiko ya gesi ya Oryx kwa kumuunga mkono Rais Dk Samia kwa kutoa majiko hayo 5000 yenye thamani ya Sh 417.5 milioni.
Awali mwenyekiti wa Chama cha Walim Mkoa wa Arusha Vumilia Joshua ameshukuru kwa Zawadi hiyo waliopatiwa na M'bunge Gambo na kuwataka serikali kuendelea kushughulikia changamoto za walimu Ili kuongeza Tija katika ufundishaji.
"Changamoto za Walimu ni nyingi lakini tumeona serikali imeanza kushughulikia hivyo tunaomba iendelee kuajiri walimu wengine kupunguza mzigo wa waliopo kufundisha mda mwingi, lakini pia ipandishe madaraja walimu na mishahara pia sambamba na kuboresha miundombinu ya kufundishia kwa Tija zaidi" amesema Mwalimu Vumilia.
Mwisho