Watoto walia na wazazi juu ya matukio ya ukatili

 


Arusha.

Wazazi na walezi nchini wametajwa chanzo cha kushamiri kwa matukio ya ukatili kwa watoto kutokana na kutelekeza majukum yao ya malezi.

Hayo yameelezwa Leo jumapili Septemba 29,224, kwenye mahubiri, nyimbo na mashairi mbalimbali yaliyowasilishwa na watoto kwenye maadhimisho ya siku ya 'Mikaeli na Watoto' katika Kanisa la KKKT Usharika wa Engarenarok ulioko Mtaa wa Bethania jijini Arusha.

Watoto hao wamesema kuwa siku hizi wazazi na walezi wao wanatumia mda mwingi kusaka fedha za kuwatunza huku jukumu la malezi wakiwaachia wadada wa kazi au ndugu zao wa karibu.

Katika mahubiri yake, Mtoto Junior James (12) amesema kuwa ndugu hao wanaoaminiwa kuwalea baadhi yao wamekuwa wakitekeleza matukio ya ukatili kwao lakini wanakosa mda wa kufikisha mambo hayo kwa wazazi wao.

"Mmekuwa busy kusaka fedha huku sisi tunaangamia, na hadi mje kugundua tumeshaathirika na mengi, Naombeni wazazi m'badilike kuanzia sasa" amesema Junior.

Mbali na hilo amewataka kubadili mfumo wa maisha wa anasa, mavazi yasiyo na staha na zaidi matumizi ya pombe kupita kiasi kwani inawafundisha kuwa ndio maisha kumbe wanapotoka.

Katika mashairi waliyoimba watoto wengine wamewashutumu pia baadhi ya wazazi kutangatanga kwenye makanisa na mikutano ya watu wanaojiita manabii na mitume kusaka upako na uponyaji.

"Mnaacha makanisa yenu ya asili mnakimbilia mahema ya watu wanaojiita manabii na mitume na bahati mbaya wakati mwingine baba anasali kivyake na mama anasali kivyake kisha mnabaki mkitugombea na kutuyumbisha kwenye Imani ya Kanisa la asili" imesema sehemu ya shairi hilo.

Katika moja ya ngonjera Gloria Siku aliwataka viongozi wa dini kurudi kwenye mafunzo na malezi ya Kikristo katika kutoa huduma ya kweli yenye msaada wa Yesu Kristo kwa lengo la kujenga Imani na Mungu wa kweli yenye kujenga hofu kwa waumini na jamii nzima ya kutekeleza matukio ya ukatili kwa watoto.

"Baadhi yenu mmekuwa mkisaka fedha kwa shida za waumini kwa kutoza fedha za maombi ya uponyaji kwa kigezo cha mapepo makubwa na madogo Ili kutofautisha viwango vya tozo, naomba muache na mumrudie Mungu wetu";amesema na kuongeza;

"Tunaomba tumrudie Mungu wa kweli maana hadi ndugu zetu sasa tunawaogopa si wanaume wala wanawake kuishi nao, kutokana na matukio ya kila kukicha tena wakitutisha kwa vipigo na matukio ya  vifo Ili kutufunga mdomo dhidi ya ukatili huu unaoangamiza Taifa" wamesema watoto hao.



Happy Mosha (11) katika moja ya Ngonjera alisema kuwa matukio ya ukatili na mauaji waliokuwa wanatizama kama sinema kwenye nchi zingine sasa yamekuwa yakitikisa kila kona ya nchi na kuzua hofu kubwa kwao.

"Hivi tumewakoseanini lakini, Ee Mungu tunusuru na watu hawa, lakini kinachosikitisha baadhi ya mama zetu na baba wamekuwa wakitekeleza pia, hivi uchungu wa kutuzaa umeishia wapi, tunaomba jamii mtulinde kwa hatma ya Taifa la Kesho" 

Mwalimu Mkuu wa shule ya mafundisho ya kidini ya jumapili kwa watoto katika Kanisa hilo , Hyness Mbasha amesema siku ya mikaeli kwa watoto ni sherehe ya kidini inayoadhimishwa na Wakristo, ili kumuenzi Malaika Mkuu Mikaeli pamoja na malaika wengine kwa kuhusishwa na vita kati ya mema na mabaya.

"Siku hii ambayo huadhimishwa Septemba 29 ya kila mwaka, mara nyingi inakuwa na maana ya sherehe ya ushindi wa mema, ujasiri, na kutetea haki. Pia inafundisha watoto umuhimu wa kuwa na nguvu ya ndani na ujasiri wa kukabiliana na changamoto" amesema Mbasha.

Mwisho.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!