Arusha
M'bunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amefanikiwa kurejesha tabasamu kwa watoto wenye ulamavu baada ya kuwakatia bima za afya zaidi ya 600 kwa ajili ya uhakika wa matibabu katika changamoto zao za kiafya.
Mbali na bima, pia watoto hao na watu wazima wamepewa msaada wa viti mwendo 600, na miguu ya bandia zaidi ya 120, lakini pia wenye changamoto ya macho wamepewa fimbo, za kutembelea.
Akizungumza kwenye hafla ya Kukabidhi vifaa hivyo, M'bunge Gambo amesema lengo ni kusaidia kupunguza changamoto wanazokumbana nazo bila vifaa hivyo saidizi.
"Lengo la bima ni kuwapatia uhakika wa matibabu kutokana na changamoto za afya za mara kwa mara wanazokumbana nazo watoto na watu wazima wenye ulemavu lakini vifaa hivyo vitapunguza mzigo wa wanaowahidumia hasa hasa katika kuwabeba kuwahamisha sehemu moja kwenda nyingine" amesema Gambo.
Amesema katika hafla hiyo, pia ameleta mitungi 500 ya gesi kwa ajili ya Walim na wazazi wanaowasaidia watoto wenye ulemavu, vyerehani nane na vitanda vyenye magodoro 20 kwa ajili ya watoto walioko kwenye vituo vya watoto yatima.
"Watoto hawa wenye mahitaji ni jukumu letu kuwasaidia kwa sababu hakuna aliyezaliwa kwa bahati mbaya hapa duniani bali Kila mtu ana nafasi yake hivyo kusaidia hivi ikawe ibada kwetu wote" amesema Gambo.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 400, Gambo amesema kuwa ni mchango kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki zake kuwasaidia wahitaji.
"Moja ya vitu ninavyojivunia ni kuwasaidia wahitaji na tangu mwaka 2000 nimekuwa nikifanya hivi na sijutii kwa sababu ni sehemu ya ibada kwangu" ameongeza Gambo.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amempongeza Gambo kwa Moyo na kuwataka wadau wengine kujitokeza kusaidia wenye mahitaji katika maeneo yao.
Mmoja wa wadau, Atul Mittal amesema wamejitokeza kusaidia kampeni hiyo ya wahitaji kutokana na sapoti kubwa wanayoipata kwa serikali kwenye shughuli zao za uwekezaji.
Nae mmoja wa wanufaika wa msaada huo, Anzirai Mohamed kutoka umoja wa wanawake wenye ualbino kata ya Sakina amesema kuwa wanashukuru kwa msaada wa vyerehani walizopata zitakazokwenda uchumi wao na familia zao.
"Awali tulikuwa na vyerehani chache na kutulazimu kuunga foleni katika shughuli zetu lakini msaada huu utatuondolea utegemezi mkubwa kwa familia zetu na sisi sasa tutakuwa tunahudumia familia zetu wenyewe" amesema Anzirai.