Arusha.
Taasisi ya Waandishi wa habari ya MAIPAC imezindua mradi wa utoaji elimu ya mpiga kura kwa mkoa Arusha unaolenga kuihamasisha jamii kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Wakizungumza katika uzinduzi wa utoaji elimu ya mpiga kura, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma alisema wanalenga kuhamasisha jamii hasa vijana kushiriki uchaguzi kwa kugombea na kupiga kura.
"Vijana mara nyingi wamekuwa wakishiriki katika mikutano ya kisiasa lakini hawajitokezi kujiandikisha kupiga kura na wale waliojiandikisha baadhi yao wamepoteza vitambulisho Sasa hii ni fursa nyingine kupata haki yao ya Kikatiba"alisema
Hata hivyo juma alisema zoezi likianza na kuboresha daftari mkoa Arusha,wanaotaka kujiandikisha au kuboresha taarifa zao haipaswi kutoa taarifa za uongo, kujiandikisha zaidi ya mara Moja.
"Lakini pia kuna Tabia ya kuuza ama kununua kadi ya mpiga kura jambo hili halipaswi kufanyika au pia hata kuharibu kadi ya mpiga kura"alisema
Meneja miradi wa Taasisi hiyo,Andrea Ngobole alisema tume huru ya uchaguzi imeandaa vituo vya kutosha vya kujiandikisha au kuboresha taarifa hivyo ni muhimu kujitokeza.
"Vituo vya kujiandikisha tayari vimetangazwa na vitafunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa 12 jioni hivyo tujitokeze"alisema
Taasisi ya MAIPAC ni miongoni mwa Taasisi ambazo zimepitishwa na Tume Huru ya Uchaguzi kutoa elimu ya mpiga kura kuanzia mwezi june mwaka huu hadi mwezi Machi mwakani.