Balozi wa Sweden awapa kibarua waandishi wa habari kuelekea uchaguzi Mkuu

 

Balozi wa Swiden Nchini Tanzania Charlotta Ozaki Macias akipokea taarifa ya hali ya waandishi wa habari kiuchumi kutoka kwa mwenyekiti wa APC, Claud Gwandu 


Arusha,

 Balozi wa Sweden Nchini Tanzania Charlotta Ozaki Macias amewataka waandishi wa Tanzania kuhakikisha jamii inakuwa na taarifa juu ya mwenendo wa maandalizi ya chaguzi zijazo zinazoendelea nchini.


Mbali na hilo pia amewataka waandishi wa habari kuhakikisha jamii inakuwa na uhuru wa kujieleza na kutoa maoni yao juu ya mwenendo wa maandalizi ya chaguzi zijazo ili waweze kushiriki kikamilifu bila walakini wala maswali.


Balozi Macias ametoa kibarua hicho jijini Arusha alipotembelea ofisi za Klabu ya waandishi wa habari Mkoani hapa, ikiwa sehemu ya ziara yake katika mikoa ya kanda ya kaskazini ya kujionea uwekezaji wa miaka 10 unaofanywa na nchi yake katika vilabu kupitia Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

 

“Swala la uchaguzi ni la wananchi wote na wanafaa kufahamu kila lilaloendelea kuanzia maandalizi hadi uchaguzi wenyewe, lakini hawawezi kujua chochote bila waandishi kupitia vyombo vya habari, hivyo tambueni mna jukumu kubwa kwao” amesema Balozi Macias

 

Amesema kuwa anatambua ziko baadhi ya changamoto zinazowakabilia waandishi nchini Tanzania, lakini zinafaa kuwa fursa za kuhakikisha wanakabiliana nazo ili jamii iweze kunufaika.

 


Tasnia ya habari inaendelea kupiga hatua katika kuhakikisha jamii inapata habari ambapo Balozi huyo amesema nchi ya Swiden haijutii kuwekeza kwenye vyombo vya habari vya Tanzania na kuahidi wataendelea kujenga vyombo vya habari vilivyo imara na vinavyojitegemea kwa ajili ya kuboresha uhuru wa kujieleza kwa wanahabari na jamii nzima.

 

"Kujenga mifumo huru, ikiwa ni pamoja na tasnia ya habari iliyoimarika kama ile ya Sweden, inachukua miaka mingi, lakini lazima muanze sasa kuchukua mifano kwa vitendo na baadae mtakuwa imara mtakavyo” Macias amewaambia waandishi wa habari na viongozi wa UTPC waliokusanyika katika ofisi ya Arusha Press Club (APC) jijini Arusha.

 

Awali, Ofisa Programu wa Ubalozi wa Uswizi anayehusika na asasi za kiraia, Steven Chimalo, alisema hali duni ya baadhi ya waandishi na ukosefu wa uhakika wa kipato imekuwa chanzo kikubwa kinachoathiri uhuru wao wa kuripoti kwa ukamilifu.

 

"Licha ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari kufanya mageuzi kadhaa, mfumo wa kisheria nao bado unaleta changamoto kwa waandishi na vyombo vya habari nchini," amesema Chimalo. 

 


Naye Mwenyekiti wa APC, Claud Gwandu amesema klabu hiyo yenye wanachama zaidi ya 60, kuanzia mwakani wanatarajia kuondokana na klabu kuendeshwa na kamati badala yake iendeshwe na bodi ya Utendaji.

 

Amesema chama hicho cha hiari kwa waandishi kimekuwa msaada mkubwa kwa wanahabari wanaopata madhila dhidi ya dola wakati wanapotekeleza majukumu yao kwa kuwasaidia mazungumzo ya suluhu au wakati mwingine wa kisheria.

 

“Zaidi tumekuwa tukiratibu mafunzo mbalimbali ya uandishi kwa ajili ya kuwasaidia kubobea katika nyanja mbalimbali” amesema Gwandu.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post