Timu ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050 yatua Arusha, wananchi waitwa kutoa maoni yao

 

Mjumbe wa Timu Kuu ya Kitaalamu ya Dira ya mwaka 2050, Dk Richard Shukia akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha 


 

Arusha.

Timu ya kukusanya maoni kwa ajili ya maandalizi ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050 imetua Kanda ya Kaskazini kwa ajili ya kuwapa fursa wananchi wa mikoa hii kutoa mchango wao wa mawazo huu ya Dira hiyo.


Zoezi hilo la ukusanyaji maoni unaoratibiwa na tume ya Mipango nchini, utafanyika kesho Jumamosi Julai 27,2024 katika kongamano la pili la kikanda kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050.



 Kongamano hilo litakalofunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa utafanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano ya AICC ulioko jijini Arusha.

 

 


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Ijumaa Julai 26, 2024, Mjumbe wa Timu Kuu ya Kitaalamu ya Dira ya mwaka 2050, Dk Richard Shukia alisema kongamano hilo linatarajia kuongeza uelewa wa umma juu ya Dira hiyo lakini pia kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuundwa kwake.

 

“Lengo la Kongamano hili kufanyika kila kanda ni ili kuwafikia wananchi wengi zaidi mubashara na kupitia vyombo vya habari ambapo tumeshafanya Kanda ya ziwa Mkoani Mwanza na sasa ni zamu ya kanda ya kaskazini Mkoa wa Arusha”amesema Dk. Shukia.

 

Amesema lengo la dira hiyo ni kutoa mwelekeo wa nchi hususani katika maendeleo hivyo kuwataka wananchi wa kanda ya kaskazini kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo.


Amesema kuwa wamefanikiwa kumshirikisha makundi yote Katika mikoa ya Kanda ya ziwa, hivyo kuyataka makundi mbalimbali ya mikoa ya Kanda ya kaskazini kuhakikisha wanachama na wajumbe wao wanafika AICC kesho kuwasilisha maoni yao.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Arusha Selemani Yusuphu amesema kuwa serikali inapaswa kujua wapi ilikwama katika dira mbili zilizopita na kutatua changamoto zilizojitokeza ili kuboresha na kufikia mafanikio iliyojiwekea katika dira mbili zilizopita.

 

“Katika dira za awamu mbili zilizopita ya mwaka 2005-2019, pamoja na ile ya 2020-2025 serikali ilikuwa na malengo mengi ikiwemo ya kuboresha hali ya maisha ya watanzania lakini pia kujenga uchumi imara unaowezesha kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine” amesema Yusuphu;

 

“Lakini ukiangalia hadi sasa mambo bado magumu, hali ya uchumi wa wananchi mifukoni ni mbaya, ajira bado ni tatizo kwa vijana ambao ni zaidi ya nusu ya watanzania wote, hivyo nadhani serikali ingeona wapi ilijikwaa na iboreshe kufanikisha hayo kwanza katika dira ijayo nadhani itakuwa vema sana” alisema Yusuph.

 

Elizabethy John Amesema kuwa dira ya Taifa ya awamu ya Tatu ilenge zaidi kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kusaidia upatikanaji wa ajira za kutosha kwa vijana lakini pia iboreshe mfumo wa Elimu nchini.

 

“Tukitoa maoni kila mara bila mafanikio kuonekana itakuwa kama tunacheza, nadhani serikali itafute ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la Ajira kwa vijana kwa kufufua viwanda vingi iwezekanavyo lakini pia kuwaongezea vijana motisha ya uwekezaji katika nchi zao”amesema Elizabethy.

 

Pia iboreshe mitaala ya ngazi zote za elimu itakayosaidia vijana wanaohitimu bila kujali ngazi gani anaweza kuona fursa ya kujiajiri, au kushindana katika soko la ajira kimataifa lakini pia aweze kutumia elimu aliyonayo kufanya uwekezaji na kuajiri wengine zaidi ya kutegemea ajira za sekta ya umma ambazo haziwezi kuajiri hata asilimia 10 ya wahitimu kutoka vyuo vyetu” amesema Elizabethy.



 

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post