![]() |
Watoto wanaodaiwa kupotea |
Arusha. Jeshi la polisi Mkoani Arusha linamsaka mtu mmoja anaejulikana kwa jina la Maiko Eliid ambae ni baba wa watoto wawili wanaodaiwa kupotea Wilayani Arumeru Mkoani Arusha kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
Hayo yamejiri baada ya kusambaa kwa taarifa za kupotea kwa watoto wawili ambao ni Mordekai Maiko(7) anaesoma darasa la tatu na Masiai Maiko(9)anaesoma darasa la Tano katika shule ya Msingi Olosiva iliyoko Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.
Tukio la kupotea kwa watoto hao lililotokea Juzi Julai 24, 2024 na kusambaa jana baada ya watoto hao kutokuonekana ndani ya masaa 24 kama ilivyohitajika na Jeshi la Polisi.
![]() |
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo |
Akizungumza na 'Habari kaskazini' Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo leo ijumaa Julai 26, 2024 amesema kuwa katika upelelezi wao wa awali wameweza kumshuku Baba wa watoto hao (Maiko) kuhusika na Tukio hilo.
“Bado upelelezi unaendelea wa kuwapata watoto hao lakini kwa hatua za awali, tunamtafuta baba yao kwanza kujiridhisha na baadae tutatoa taarifa iliyokamilika” amesema Kamanda Masejo.
Amesema kuwa sababu kubwa ya kumshuku baba wa watoto ni kutokana na kujirudia kwa tukio hilo kama ilivyokuwa awali mwaka mmoja uliopita.
“Tunamshuku baba huyo, kwa sababu sio mara ya kwanza watoto hawa kudaiwa kupotea” amesema Masejo na kuongeza;
“Mwaka jana watoto hawa walidaiwa hivyo hivyo kupotea na katika kuwatafuta tukawakuta wako salama na baba yao wilayani Karatu, hivyo kwa sasa tunashuku kuwa itakuwa hivyo hivyo” amesema Masejo.
Akizungumzia tukio hilo, Mama wa watoto hao, Elizabeth Modesta (31) amesema kuwa hata yeye amepata taarifa za watu wa karibu na ndugu wa aliyekuwa mumewe kuwa baba yao amewachukua watoto wake na amevuka nao kwenda Nchini Kenya.
“Kwa taarifa inavyoonekana, baba yao ndio kawachukua na kwenda nao nyumbani kwao huko Kenya anakoishi kwa sasa baada ya mimi na yeye kutengana” amesema Mama huyo.
Elizabeth ametumia nafasi hiyo kuiomba serikali kumsaidia kurudisha watoto wake kwani hawezi kuishi nao mbali na watatengeneza utaratibu wa wazazi wote wawili kuwaona wazazi wao.
“Mimi ninachoomba nisaidiwe watoto wangu warudi na kama atakuwa anataka kuwaona basi atawachukua kipindi cha likizo na kuwarudisha kwa ajili ya shule lakini siwezi kuishi bila wanangu” amesema Elizabeth.
Awali Akizungumza na 'Habari Kaskazini ', Elizabeth alisema kuwa siku ya jumatano watoto wake wamepotea katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuagana nao na kuwapandisha daladala kwenda shule lakini hawajarudi na alipofuatilia shuleni ilibainika pia kuwa hawakufika shule ndipo kutoa taarifa Polisi na upelelezi kuanza.