Bertha Mollel, Arusha
Mwanariadha wa kimataifa kutoka Tanzania Magdalena Shauri anaeshikilia rekodi ya Taifa ya mbio ndefu amesema kuwa baada ya medali ya Shaba ya Berlin Marathon, kwa Sasa mazoezi yake makubwa yanalenga kwenye mashindano ya Olympic.
Shauri aliyefuzu kushiri mbio hizo hivi karibuni, ameahidi kuongeza nguvu katika mazoezi Ili kuhakikisha anavuna medali ya dhahabu katika michuano ya Olympic mwaka 2024 itakayofanyika Paris Ufaransa.
Magdalena ameyasema hayo baada ya kutwaa medali Shaba katika mashindano ya Berlin marathon yaliyofanyika September 24 akitumia saa 2:18:41.
Mbali na kuwa mtanzania wa kwanza mwanamke kuchukua medali hiyo kwa kutumia mda aliotumia lakini pia imemfanikisha kufuzu kushiriki michuano ya Olympic akiungana na mwanariadha Alfonce Simbu na Gabriel Geay.
"Haikuwa rahisi hata kidogo, kwani nilikuwa katika presha kubwa kuhakikisha mwaka huu nafanya kitu kupitia mchezo wa riadha, lakini mwisho namshukuru Mungu nimefanikiwa kumaliza nafasi ya tatu"
Alisema kuwa malengo yake ilikuwa kumaliza nafasi ya kwanza lakini dakika za mwisho mashindano yalikuwa magumu kutokana na Kila mmoja kuitaka nafasi hiyo.
"Nilipambana sana hadi kiwango changu cha mwisho lakini mambo ndivyo mambo yalivyo sitaki kurudi nyuma kwa sasa ninarudi kambini kuendelea na mazoezi kuhakikisha nailetea nchi yangu heshima ya medali katika michuano ya Olympic mwakani nchini Ufaransa" alisema Magdalena.
Katibu wa Chama cha riadha mkoa wa Arusha, Rogath Steven alisema Arusha na Tanzania zinaweza kutwaa medali nyingi zaidi katika mbio za kimataifa endapo wadau wa riadha wataunga mkono maandalizi yote kuanzia kambini.
"Tunachohitaji ni kuungwa mkono, tunawaomba wadau kuungana nasi ili kuhakikisha kwanza tunawaandaa wanariadha wetu wafuzu wengi zaidi kwenye mashindano haya ya Olympic lakini pia baadae tutakapoanza kambi wapate sapoti ya kuwezeshwa Ili wakafanye vema huko na kuleta medali nyingi zaidi"
Kwa upande wake Kocha wa Magdalena, Anthony Muingereza alisema Siri ya mafanikio ya mwanariadha wake ni mazoezi, nidham, lakini pia sapoti kubwa anayopata kutoka kwa viongozi wake kazini (JWTZ).
Magdalena alinyakua medali ya shaba nyuma ya Muethiopia Tigist Assefa aliyejinyakulia dhahabu baada ya kukata utepe wa kilomita 42 kwa saa 2 : 11 : 53 na mwanariadha wa Kenya Sheila Chepkirui aliyetwaa fedha akimaliza kwa saa 2 : 17 : 49
Mwisho...