Waziri Ndumbaro aagiza matumizi ya Tehama kutumika katika mifumo yote ya kisheria ili kusaidia jamii kwa urahisi

 

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt Damas Ndumbaro akifungua kikao kazi cha mafunzo ya matumizi ya mifumo ya Tehama kwa Wasajili wasaidizi wa huduma za sheria, inayofanyika Arusha kwa siku mbili octoba 17 na 18, 2022


 Na Bertha Mollel , Arusha

 

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt Damas Ndumbaro  amewaagiza wasaidizi na wataalamu wa kisheria kutumia mifumo ya teknolojia  ya habari na mawasiliano (Tehama), katika kutoa misaada ya kisheria ili kuweza kusaidia jamii kubwa  kwa haraka na wepesi zaidi.

 

Waziri Ndumbaro ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha mafunzo ya matumizi ya mifumo ya Tehama kwa Wasajili wasaidizi wa huduma za sheria, maafisa magereza, taasisi za huduma za msaada wa  sheria, wataalamu wa sheria na watumishi kutoka Tamisemi kinachofanyika mkoani Arusha kwa siku mbili.

 

“Matumizi ya Tehama yakitumika zaidi katika kutoa elimu au misaada ya kisheria inarahisisha mambo mengi ikiwemo hata kuokoa mda wa kuzifuata huduma hizo maofisini lakini pia foleni katika ofisi hizi zitapungua na wananchi kuona faida na umuhimu wenu”

 

Alisema wizara yake inasisitiza matumizi ya Tehama pia katika kipindi hiki zaidi ambacho wananchi wanadai katiba mpya ambayo mifumo  hii itasaidia kujua katiba iliyopo, inafanya nini na ina mapungufu gani na yapi ambayo yanafaa kufanyiwa maboresho.

 

“Huwezi kudai katiba mpya bila kujua ina mapungufu gani hivyo hakikisheni wananchi wanayapata hayo huko huko walipo  kwani wakishajua ndio wataweza kudai haki yao vizuri” alisema Ndumbaro na kuongeza…

 

“Bajeti ya mwaka 2022/2023 Wizara yangu  imeweka vipaumbele 14,  ikiwemo matumizi ya tehema, katika mifumo yote ya sheria ili matumizi yote yaende kidigitali na niwapongeze watoa huduma za kisheria mmeanza kutumia”

Waziri Ndumbaro, alisema Mhimili wa mahakama umefanikiwa sana katika matumizi ya Tehama likifungamanishwa na haki kupatikana kwa haraka na kuondoa usumbufu.



Awali akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria, Kaimu Katibu tawala mkoa wa Arusha, David Lyamongi, alisema kuwa Mawakili binafsi wamekuwa ni msaada mkubwa katika maswala ya kisheria ambapo wamekuwa wakitumika kutatua kesi mbalimbali kwa wananchi na hivyo kuondoa usumbufu na haki kupatikana .

Amesema kuwa kupitia mawakili hao Yatima na Wajane wamekuwa  wakipata msaada hivyo umefikawakati wapewe kipaumbele na nguvu ya kisheria ili kuweza kukamilisha kazi yao kwa wakati.

Nae mkuu wa Kitengo cha Tehama wizarani, Gabriel Omary, amesema mafunzo hayo ya utumiaji wa huduma ya Tehama  yana lengo la kuwezesha wananchi kutumia huduma ya mtandao ilikuweza kupata haki kwa wakati na haraka ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia gharama pindi wafuatapo huduma za kisheria.

Baadhi ya washiriki wa 
mafunzo ya matumizi ya mifumo ya Tehama kwa Wasajili wasaidizi wa huduma za sheria, inayofanyika Arusha kwa siku mbili octoba 17 na 18, 2022

“leo tunawanoa zaidi wenzetu wanaotoa misaada ya kisheria katika taasisi mbali mbali mbali za magereza, uhamiaji, polisi, tamisemi kwa ajili ya kutambua namna ya kutumia mfumo wa Tehama kusaidia jamii hasa maswala ya kisheria ambapo tunatarajia wananchi watanufaika nazo”

 

Baadhi ya washiriki wa 
mafunzo ya matumizi ya mifumo ya Tehama kwa Wasajili wasaidizi wa huduma za sheria, inayofanyika Arusha kwa siku mbili octoba 17 na 18, 2022


 

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!