Na Mwandishi wetu , Habari Kaskazini
Arusha . Shirika lisilo la kiserikali la WAMATA limefanikiwa kuwatua wanawake wa Bwawani ndoo kichwani baada ya kuwajengea mradi mkubwa wa miundo mbinu ya maji uliogharimu jumla ya milioni 100.
Shirika hilo lisilo la kiserikali linalojihusisha katika kuwasaidia watu wenye VVU na Ukimwi nchini Tanzania (Wamata) limejenga mradi huo katika kata ya Bwawani iliyoko wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Mradi huo uliohusisha uchimbaji wa kisima kirefu uliowekewa matanki ya kuhifadhia maji pamoja na vituo vya kuchotea maji unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wakazi 20,000 wa kata ya Bwawani,shule na zahanati ya Themi ya Simba yenye wodi za wanawake za kujifungulia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Wananchi hao walisema kuwa wameishi miaka mingi bila kuwa na uhakika wa kupata maji Safi na salama hivyo kuoshukuru shirika hilo kwa kuwaonekania.
"Tunashukuru Sana kwa msaada wenu jamani, wake zetu wameteseka sana kufuata maji ya mabwawa na vidimbwi lakini leo tumepata maji ambayo yatatusaidia hata kwenye zahanati yetu ambayo kina mama wajawazito walikuwa wanakosa maji kwa usafi wao wakati wa kujifungua" alisema Joseph meing'ori
Happy Kaaya, alisema kuwa, adha ya maji katika kitongoji hicho iliwapoteza muda mwingi wa kutembea umbali wa zaidi ya Kilometa 5 kutafuta maji, jambo ambalo lilidhoofisha hali ya afya na uchumi wa familia zao.
"Sisi wanawake tumepata mkombozi, sisi ndio tulikuwa wahanga wakubwa wa ukosefu wa maji, tulitumia muda mrefu kutafuta maji, tunashukuru Serikali kukubali wafadhili hawa watutekelezee huu mradi kwetu"
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa maji, Mkurugenzi wa shirika la WAMATA, John Tarimo alisema kuwa shirika hilo kwa ufadhili wa shirika la World Server la nchini Marekani, limefanikisha mradi huo wa maji, mara baada ya kuona adha kubwa ya maji iliyokuwa inawakabili wananchi wa Bwawani hususani kijiji cha Themiyasimba.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha Selemani msumi amewashukuru wadau wa shirika hilo kwa kutoa huduma hiyo muhimu kwa wananchi wa Themiyasimba, ikiwa ni utekelezaji wa malengo ya Serikali ya awamu ya sita ya kumtua mama ndoo.
"Serikali inathamini kazi zinazofanywa na wadau za kufanikisha vipaumbele vya Serikali, WAMATA mmewezesha kumtua mama ndoo ikiwa ni sera ya Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na mama Samia Suluhu Hassan". Amesisitiza Mkurugenzi Msumi
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Themiyasimba, Mhel Mussa Msengi, ameshukuru kwa mradi huo wa maji, kwa kuwa changamoto ya maji ilikuwa ni tishio kubwa la afya kwa wananchi walio wengi.
"Wananchi walikuwa na uhitaji mkubwa wa maji safi na salama, hivyo tunaomba kama inawezekana, kuongezewa tanki lingine ili maji yawafikie wananchi wengi zaidi katika vijiji vya jirani, kwa kuwa kisima hicho kina maji mengi na ya kutosha ". Amesisitiza Mwenyekiti huyo wa kijiji.
Awali shirika la WAMATA licha ya kutekeleza mradi wa maji, lakini pia limeanza kuwahudumia vijana 10 watakaopewa mafunzo ya ushonanaji na kuchomelea vyuma lengo kuu ni kupambana na ukosefu wa ajira nchini.