Bertha Mollel, Arusha
Kampuni ya kitalii ya Zara tour imeanza kampeni yake maalum ya kuhamasisha wananchi kuadhimisha miaka 61 ya uhuru wa Tanzania kwa kupanda mlima Kilimanjaro katika kuhamasisha utalii wa ndani.
Mlima huo ulioko ndani ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro ndio unaongoza Kwa urefu barani Afrika ambapo Kilele cha Kibo kina urefu wa mita 5895 ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi kwa sababu ya kufunikwa na theluji mwaka mzima.
Katika mlima huo pia kuna vilele vingine viwili ukiachia huo wa Kibo pia kuna Shira, upande wa magharibi, kikiwa na urefu wa mita 3962, Mawenzi upande wa mashariki, chenye urefu wa mita 5149
"Huu mlima upo kwetu, tusishuhudie tu wageni wakija kuupanda, hivyo niwasihi watanzania wajitokeze kujisajili kwetu Kwa ajili ya kuupanda mlima Kilimanjaro, safari tutakayoianza desemba 4 mwaka huu hapa mjini Moshi" alisema mkurugenzi wa Zara Tour Zainab Ansell.
Alisema kuwa kampeni hiyo ya kuhamasisha watu kujitokeza kupanda mlima Kilimanjaro kama sehemu ya kuadhimisha miaka 61 ya uhuru wa Tanzania, una lengo la kumuunga mkono Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kukuza utalii.
"Rais Samia anafanya mengi kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara wa utalii Afrika ndio maana akafikia hadi kutengeneza filamu ya Royal tour, hivyo sisi kama wadau tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunabuni kampeni nyingi za kumuunga mkono" alisema CEO Ansell
Alisema kuwa Tanzania ina vivutio vingi ambavyo bado havijatangazwa ipasavyo Ili kuvutia watalii wengi zaidi katika kufikia azma ya serikali ya 2025 ya kufikisha watalii milioni tano watakaoiingizia Taifa zaidi ya Dola billion 6.
"Wadau wa utalii na Taasisi binafsi na za serikali zinazofanya kazi za utalii yapaswa tushirikiane kuhakikisha vivutio vyetu vinatangazwa kwani zipo ambazo hazijafikiwa kutangazwa lakini hata zilizotangazwa hazijakidhi vigezo vya kumvuta mtalii kuweka bajeti ya mpya Kwa ajili ya bidhaa hizo" alisema Ansell.
Aidha Tanzania inatarajia kuadhimisha miaka 61 ya uhuru desemba 9 mwaka huu ambapo awali ilikuwa ni kushusha chini bendera ya mkoloni na kupandisha bendera ya Taifa juu hasa mlima Kilimanjaro.