Rais Samia atoa bil. 2 kujengwe madarasa 100 jiji la Arusha, DC Mtanda atoa mkwara mzito


 Bertha Mollel , Arusha


 Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekabidhi Jumla ya shilingi billion 2 Kwa halmashauri ya jiji la Arusha Kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 100 ndani ya siku 75.


Akizungumza Wakati wa ukabidhi wa fedha hizo Kwa niaba ya Rais, mkuu wa wilaya ya Arusha Said Mtanda amesema kuwa fedha hizo zinalenga kutatua Kero ya uhaba wa madarasa Kwa wanafunzi wa kidato Cha kwanza watakaochaguliwa msimu ujao wa mwaka 2023.

"Maelekezo ya hizi fedha ni kujenga madarasa 100 ndani ya shule 20 za jiji la Arusha Kwa muda wa siku 75 muwe mmekabidhi mradi Kwa ajili ya ukaguzi wa ubora na maelekezo mengine lengo la serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wa kidato Cha kwanza watakaochaguliwa wanaanza pamoja wasikose pa kusomea Wala wasibanane" alisema Mtanda

Katika utekelezaji wa mradi huo, Mtanda amemtaka mkurugenzi wa jiji la Arusha kutumia muda wa siku Saba pekee kuunda kamati ya kusimamia mradi huo na kufanya tathmini ya manunuzi itakayozingatia bei nafuu.

"Nataka muunde kamati itakayohusisha wataalamu wa ujenzi, wazazi na viongozi itakayokuwa na meno ya kusimamia kuhakikisha mradi huu unatekelezwa vizuri bila kuyumbishwa na ukamilike na kukabidhiwa Kwa Wakati"

Mtanda akitoa onyo dhidi ya matumizi mabaya ya fedha hizo akisema kuwa serikali itawachukulia hatua Kali za kisheria watakaobainika kufanya ubadhirifu wa aina yoyote Kuanzia kwenye manunuzi hadi utekelezaji.

"Hizi fedha zimeletwa sio sadaka, ni za kazi aliyokisudia mheshimiwa Rais zikatatue Kero, Sasa nyie nendeni mkafuje mtakiona Cha moto, nataka Kila darasa lijengwe Kwa milioni 20 na siku ikikabidhiwa iwe na hadhi, yenye ubora na uhalali wa Hali ya juu huku mkishirika wazazi na wanafunzi juu ya utekelezaji huu alioahidi Rais na ametekeleza" alisema DC Mtanda.

Kwa Upande wake mkurugenzi wa jiji la Arusha Hargeney Chitukuro alithibitisha kupokea fedha hizo zilizoingizwa kwenye akaunti ya jiji la Arusha akisema kuwa tiyari wamezielekeza kwenye shule zilizoonekana kuwa na uhitaji.

Alisema kuwa kila shule zimeelekezwa kutumia milioni 20 Kwa darasa moja hadi kukamilika kwake,  ambapo alizitaja shule zitakazonufaika  na idadi ya madarasa yatakayojengwa kuwa ni Arusha day, itakajenga madarasa 5, Arusha sekondari (8), Terrat (7), na  Elerai (8).

"Shule zingine ni Felex Mrema (2), Kaloleni (5), kimaseki (3), Lemara(2), Mkonoo  (1) na zingine ni  Moivaro (2), Mrisho Gambo (4), Muriet (11), Naura (5), Ngarenaro (5), Olasiti (5), Olmoti(3), Olorien (1), Sinoni, (14), Sombetini (4) na Unga Ltd (3)".

Alisema kuwa baada ya ujenzi huu, tatizo la uhaba wa madarasa litakuwa limekwisha katika jiji la Arusha baada ya hivi karibuni kufanikisha ujenzi wa madarasa 105 kupitia fedha za uviko - 19 Kwa gharama ya shilingi 2.1.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!