Mchungaji Mkemwa akemea wanaojibadili maungo yao kwaajili ya urembo.

 

Arusha 

Mchungaji kiongozi wa kanisa la KKKT usharika wa Engarenarok mtaa Bethania Herbert Amon Mkemwa amesema kuwa watu wanaojibadili maungo yao kwa ajili ya urembo ni kujifanyia ukatili wa miili yao lakini pia na imani yao.

Amesema mbali na wanaobadili maungo yao pia wanaobadili jinsia zao za asili au matumizi yake wamekuwa chukizo mbele za Mungu kitendo ambacho kinafaa kupingwa na watu wote kwani kushamiri kwake kutaleta athari kubwa kwa kizazi kijacho.

Mchungaji Mkemwa aliyasema hayo wakati akihubiri kwenye ibada ya jumapili yenye somo la kukemea vitendo vya ukatili vinavyoendelea nchini.

“Siku hizi watu wanamrekebisha hadi Mungu eti wanaenda kujirekebisha maungo yao kwa kuongeza makalio, matiti na hata tumbo, niwaambie huo ni ukatili maana Mungu alikupa kwa kipimo chako kulingana na hitajio, sasa unapokwenda kubadili sijui unataka nini kama si kujikatili”

“Ndio maana nasema kuna watu ukatili wameanza kujikatili wao wenyewe kabla ya kukatili wengine, niwaombe tumrudie Mungu nae atatuwezesha kushinda haya majaribu” amesema.

Mbali na hilo amekemea watu wanajibadili maumbile yao ya asili au matumizi yake, akisema kuwa inahatarisha ustawi wa kizazi cha sasa na baadae.

“Kuna mda laana inachukua dunia na kutupitisha kwenye mapigo ikiwemo ukame, njaa, mafuriko na mambo mengine kumbe kwa sababu ya ukatili ambao tunafanya kwa watu wetu na kwetu wenyewe”

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake katika Kanisa hilo,Niwaeli Minja amesema kuwa wameanzisha mpango wa kuelimisha watoto na vijana kuhusu athari za vitendo vya kinyume na maadili.

"Mpango huu unalenga kuwakinga watoto wa kiume na wa kike dhidi ya ubakaji, ulawiti, na mimba za utotoni"amesema na kuongeza;

"Zamani tulidhani watoto wa kike pekee ndio wako hatarini, lakini sasa hata wavulana wako katika hatari kubwa, ndio maana  tumekuja na mpango wa kuwafundisha kuvunja ukimya ili waweze kuripoti matukio ya ukatili kabla ya kuzoea na kuona ni jambo la kawaida," amesema Minja.

Akizungumzia hali hiyo mmoja wa waumini Godlisten lema ameiomba serikali kuona umuhimu wa kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaobadili maumbile yao au matumizi yake ya asili kwa madai kuwa kikithiri kwake kunazidi kuhatarisha mustakabali wa kizazi kijacho.

Amesema kuwa maumbile ya binadamu ni kazi ya Mungu, hivyo kitendo cha kubadili jinsia au matumizi ya viungo vya mwili ni tendo la kujidhuru na kujifanyia ukatili lakini pia kuharibu asili yake.

"Serikali ione umuhimu wa kuadhibu hawa watu kisheria kwasababu mfikirie mwanamke anayejibadili kuwa mwanaume au kuwa na mahusiano na mwanamke mwenzake, hapo unategemea watazaana kuijaza dunia vipi? Au mwanaume anayekata umbile lake na kujiwekea la kike, unadhani atazaa mtoto wa aina gani hata kwa msaada wa teknolojia?" amehoji Lema.

Mwisho…


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post