Arusha.
Zaidi ya wananchi 300 kutoka kijiji cha Engaruka Chini wilayani Monduli wameandamana kupinga uongozi wa mwenyekiti wao kwa madai ya kuuza maeneo ya akiba kwa wawekezaji bila kufuata taratibu au kuwashirikisha wananchi.
Maeneo yanayodaiwa kuuzwa yapo jirani na eneo la ekari 60,884 zilizotengwa baada ya serikali kulipa fidia ya zaidi ya Sh 14.4bilioni ili kupisha uwekezaji wa viwanda viwili vikubwa vya magadi soda vyenye thamani ya Sh1.6 trilioni.
Uwekezaji huo unakuja baada ya Tafiti kubaini kuwa eneo hilo lina akiba ya magadi soda inayofikia mita za ujazo bilioni 3.8, sawa na tani milioni 787.
Katika maandamano hayo, yaliyokuwa yakielekea kufunga ofisi ya kijiji kabla ya kuzuiwa na mjumbe wa serikali ya kijiji, Maria Legasta, wananchi walieleza kusikitishwa na mwenyekiti huyo kwa kuvunja ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wake Novemba mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa wananchi hao Happyness Samweli amesema kuwa awali mwenyekiti huyo wakati wa kampeni aliahidi kusimamia ardhi ya kijiji isiuzwe hovyo kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma sambamba na kutataua kero zingine za migogoro ya ardhi.
“Cha kushangaza ameshika ofisi hata miezi sita hana ameanza kutusaliti na kuuza maeneo ya akiba ambayo yametengwa ajili ya makazi (Muaten)";
"Tena anauzia watu wasio wakazi wa hapa kijijini bila kufuata taratibu zozote ikiwemo kushirikisha wananchi jirani wa eneo husika wala vikao vyovyote vya kuelezea sababu ya uuzaji wala mapato na matumizi ya hizo fedha hakuna” amesema.
Kutokana na hayo tunaomba serikali ituondolee huyu mtu maana tumemkataa kwa kauli moja hatumtaki na wala asitekeleze shughuli zozote za uongozi wa kijiji chetu maana amekuwa msaliti.
Nae Neema Mollel amesema kuwa maeneo hayo yameanza kuuzwa kiholela mwaka huu baada ya serikali kuonyesha nia ya kutaka kufanya uwekezaji wa ujenzi wa magadi soda ambapo baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakimiminika kila kukicha kununua ardhi karibu na maeneo hayo kwa ajili ya kufanya nao uwekezaji.
"Maeneo ambayo watu wanakuja kuwarubuni viongozi wetu kununua ni haya yanayozunguza ardhi ambayo serikali imechukua kwa ajili ya kuwekeza viwanda vya magadi soda, sisi hatukatai uwekezaji lakini kwanini hatushirikishwi mwisho tutauziwa hadi tunamoishi tutaenda wapi jamani” amesema.
Nae Samwel loosikito amesema kuwa kilio kingine ni tuhuma ambazo mwenyekiti huyo wa kijiji ameorodhesha watu 42 kwa ajili ya kuwa sehemu ya mgawo wa fidia kiasi cha sh 14.4 ambazo serikali imetoa kwa wananchi wa vijiji vinne wanaoishi eneo hilo kupisha.
“Baadhi yao hawajapewa fidia zao zaidi ya mwenyekiti kuwapa fidia baadhi ya watu na wengine wakitakiwa kuondoka eti fidia zao zitawafuata lakini hadi leo hawajapewa”.
Mwaanchi Mwingine Nangakwa Siwandeti amesema kuwa kutokana na hilo hawatakubali mradi wowote utekelezwe katika maeneo yao ikiwemo wa biashara ya kaboni ambayo baadhi ya maeneo ya malisho yamewekwa alama (Bikon) kwa ajili ya utekelezaji kuanza.
“Juzi yenyewe tumesikia eti kuna mradi mwingine wa kuuza hewa, sisi tunasema hatujui uuzaji wa hewa ya Mungu tuliyopewa tuvute wala faida yake hivyo huu mradi hatutakubali utekelezwe katika eneo letu”.
Akizungumza wakati wa kuwatuliza wananchi hao, Mjumbe wa serikali ya kijiji hicho Maria Lagasta amewataka wananchi hao kuepuka kufanya vurugu na kuharibu mali za serikali akiahidi kushughulika na kero hizo.
“Kuandamana sio suluhisho wala sio utatuzi wa kudumu wa kero zenu, mimi naishi katika eneo hili na mnanijua vema naombeni mrudi katika makazi yenu na mimi kero ninazochukua na kufikisha ofisi ya kata na kwa Mkuu Wilaya kwa taratibu zingine za kushughulikia” amesema.
Mwenyekiti anaetuhumiwa kuuza maeneo hayo, Koning'o Mollel amesema kuwa hakuna ardhi iliyouzwa katika eneo lake huku akigoma kutoa maelezo zaidi akidai waandishi wamevamia eneo la utawala wake.
“Siwezi kuongelea hayo mnayotaka kwa sababu kwanza mmekuja kusikiliza kero za wananchi wangu bila kibali kutoka katika ofisi ya kijiji hilo ni kosa kubwa kuja eneo la utawala wangu bila taarifa na kuongea na wananchi wangu bila kibali changu kama kiongozi wao hayo ni makosa makubwa mmefanya”;.
“Hivyo endeleeni na kazi yenu sina cha kuwajibu kikubwa mjue hakuna ardhi imeuzwa katika kijiji cha Engaruka chini ya uongozi wangu na mkitaka zaidi mkajipange mje kiofisi siku nyingine” amesema.
Mkuu wa Wilaya atuma timu ya uchunguzi, huku akionya wanaotaka kuhujumu mradi wa magadi soda.
Akizungumzia swala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga amesema kuwa amepata taarifa za mgogoro huo na amekwisha kutuma timu ya uchunguzi kubaini ukweli wa mambo hayo.
“Niko safarini, lakini timu yangu nimetuma ikafanye kazi hiyo ya kuchunguza kujua ukweli wa tuhuma hizo na kama ikibainika mwenyekiti amehusika kwa namna yoyote ajue tutamshughulikia” amesema.
“Pia kama kuna mtu au muwekezaji yoyote amemlipa hela mwenyekiti kwa ajili ya kununua ardhi ya serikali basi ajue amepata hasara maana hiyo hela itakuwa amempa mwenyekiti hela ya matumizi sio ya kununua ardhi kwani taratibu zote za kijipatia ardhi zinafahamika” amesema Kiswaga.
Kiswaga ametumia nafasi hiyo kuwataka mashirika na taasisi binafsi wakiwemo wanasiasa na wananchi wote ambao wanajaribu kuhujumu uwekezaji huo wa magadi soda kuwa serikali haitawaacha salama.
“Na nitoe onyo mapema kwa wananchi na mashirika binafsi maana zipo NGO’S ambazo vimeanza kupotosha swala la uwekezaji huu, nao wakibainika kwa kweli tutawachukulia hatua maana mradi sio wa manufaa ya monduli pekee bali kwa wananchi wote mkoa na nchi kwa ujumla”;
“Pia kuna wanasiasa wamejiingiza hapo katikati tumesikia na tutawatafuta na kukaa nao mezani tujue kabisa wanataka nini kwani nao ni wadau lakini siasa za kupotosha hatutakubaliana nalo, bali tunataka zinazojenga mafanikio ya huu mradi kwa asilimia zote” amesema DC Kiswaga.
Kiswaga pia amewataka wananchi ambao hawajapata fidia wafuate taratibu wapate fedha zao kwani serikali ilishatoa kwa ajili ya ulipwaji fidia wananchi 595 kutoka vijiji vinne vya Engaruka Chini, Mbaash, Idonyonado na Irerendeni