Arusha.
Arusha .Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko ameikabidhi Benki ya NMB tuzo maalum ya heshima kwa kutambua mchango wa Taasisi hiyo ya kifedha katika kuifanikisha maandalizi ya mkutano wa 16 wa Ununuzi wa Umma (PPPRA) katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Biteko ametoa tuzo hiyo kwa NMB, wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo unaoshirikisha zaidi ya wataalamu 1000 wa manunuzi ya umma na ugavi kutoka nchi saba za jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano (AICC) kwa siku nne mfulululizo, kuanzia leo Septemba 9-12, 2024.
Katika Mkutano huo Biteko amewataka wataalamu wa manunuzi ya Umma kuhakikisha wanajadili na kupata muafaka wa kuhakikisha mifumo yao inasomana ili kuweza kudhibiti wizi wa fedha za umma.
Amesema Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi wa umma (PPPRA)kama chombo cha udhibiti wa manunuzi inayolenga kufanya mageuzi na kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma inafaa kuingia pia katika mashirikiano katika nchi zote.
"Lakini kama mnavyotambua zaidi ya asilimia 70 ya fedha za bajeti zinaelekezwa kwenye sekta ya manunuzi ya umma, basi yafaa mfanye kazi yenu kwa uadilifu mkubwa, weledi na uwajibikaji wa hali ya juu ili kuleta mafanikio katika nchi zetu" amesema Biteko
Akizungumzia tuzo waliyoipata, Mkuu wa Idara ya huduma za kibenki kwa serikali na Ofisi ya Makao Makuu ndogo ya NMB, Vicky Bishubo aliishukuru serikali kwa kutambua mchango wao wa kudhamini mkutano huo.
“Tumefanya hivi kwa kutambua sekta ya manunuzi katika maendeleo ya nchi yetu hasa kwa kufuata maadili, weledi na uwajibikaji inavyoweza kusaidia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza kiwango cha fedha katika mzunguko” amesema Vicky.
Amesema kuwa tuzo hiyo inawahamasisha kuendelea kuwahudumia wananchi na serikali kwa ujumla hasa katika kutatua changamoto mbalimbali za kifedha na pia katika kuendelea kubuni mazao mengine ya kusaidia jamii.
“Mbali na hili tunaendelea kuhamasisha matumizi ya kidigitali katika manunuzi ya umma lakini pia kusaidia dhamana kwa wakandarasi na wazabuni bila kuweka mali reheni ili kufankisha shughuli zao na kupata tenda pia”
Awali Mkurugenzi wa PPPRA, Dennis Simba alisema mkutano huo una lengo la kujadiliana na kubadilishana uzoefu juu ya maswala ya manunuzi ya umma lakini pia matumizi ya teknolojia katika kufanikisha shughuli zao.