Arusha Jumla ya wanafunzi 51 wamepata Ufadhili wa masomo ya mitaala ya kimataifa katika shule ya Arusha Meru.
Ufadhili huo wenye thamani ya sh 125 milioni, wanafunzi hao wamepata baada ya kuongoza kwenye mitihani yao ya kuwania nafasi ya kufadhiliwa.
Mitihani hiyo ya kitaaluma, iliyoshindaniwa na wanafunzi zaidi ya 1000 kutoka shule mbalimbali nchini, ni kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita.
![]() |
Mwenyekiti wa bodi ya shule Arusha Meru international, Kake Radhiwal |
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo ya Arusha Meru, Kake Radhiwal amesema lengo la mashindano ya Ufadhili huo ni kuwapa nafasi wanafunzi wasioweza kugharamia mitaala hiyo na wana vipaji vya kitaaluma kupata nafasi ya kuchukua masomo ya mitaala ya kimataifa. |
"Hii ni kwa ajili ya kuiunga mkono pia serikali kuhakikisha dhana ya kukuza elimu ya Tanzania inafanikiwa ndio maana tumewapa wanafunzi wenye vipaji vya kitaaluma kutoka Tanzania ufadhili wa kusoma hapa shuleni kwetu” amesema.
![]() |
Mkurugenzi wa shule ya Arusha Meru International, Dk Zeeshan Khan |
Mkurugenzi wa shule ya Arusha Meru International, Dk Zeeshan Khan amesema kuwa katika shule hiyo waliobobea zaidi katika masomo ya Sayansi, wanatarajia wanafunzi waliopo kwenye Ufadhili huo watafanya vizuri zaidi katika masomo na kutimiza ndoto zao.
"Sasa hivi Dunia inaelekeza ajira na fursa za kiuchumi kwenye ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia hivyo lazima tuwekeze sasa kwa wanafunzi wetu kulitambua soko mapema " amesema.
Nae Mmoja wa wanafunzi waliofanikiwa kupata ufadhili huo, Joan Samwel Rugemalila wa kidato cha nne kutoka shule ya Precious Blood amesema kuwa ufadhili huo utamsaidia kumpunguzia mzazi wake mzigo wa kulipa ada.
“Mtihani ulikuwa mzuri, ingawa mgumu lakini unajibika hivyo nimefurahi kupata nafasi hii ambayo nimempunguzia mzazi wangu mzigo wa kulipa ada lakini pia naamini nitatimiza malengo yangu zaidi ya kufanikisha kubobea katika maswala ya sayansi na baadae kuwa daktari wa magonjwa mbalimbali ya binadamu" amesema Joan.